Watu 424 kati ya 447wabainika kuugua presha

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 04:56 PM Mar 24 2024
Ofisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Bukoba (BRRH) Ernest Lengesela akimpima kipimo cha kuangalia shinikizo la damu mwilini mwananchi aliyefika katika hospitali hiyo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Ofisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Bukoba (BRRH) Ernest Lengesela akimpima kipimo cha kuangalia shinikizo la damu mwilini mwananchi aliyefika katika hospitali hiyo.

WATU 424 kati ya 447, waliofanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo, mkoani Kagera, wamebainika wanaugua presha.

Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Yona Gandye, amesema.

Amesema asilimia 95 ya watu waliowafanyiwa vipimo waliwakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu (presha).

“Watu 447 wakiwamo watu wazima 405 na watoto 42 wamepata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu mkoani Kagera.

“Kambi hiyo ya siku tano ilifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI, kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Bukoba (BRRH),” amesema.

“Baadhi yao tuliowakuta na tatizo la shinikizo la damu walikuwa  na matatizo mengine ya moyo, ikiwamo moyo kutanuka, uwezo wa moyo kusukuma damu kuwa chini.

“Wengine walikuwa na shida katika utengenezaji wa mapigo ya moyo na hivyo mapigo yao ya moyo kuwa chini kuliko kawaida,” ameeleza Dk. Gandye.

“Watoto tuliowapima baadhi yao tumewakuta na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu kwenye moyo na mishipa ya damu.”

Amesema wagonjwa 55 wakiwamo watu wazima 50 na watoto watano, ambao wamekutwa na matatizo ya moyo, wamepewa rufani ya kwenda kutibiwa JKCI.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Bukoba, Dk. Museleta Nyakiroto, ameishukuru JKCI kwa kuwa, imewajengea uwezo wataalamu wa BRRH katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo.

“Tutaendeleza uhusiano uliopo baina ya JKCI na BRRH na ninatarajia upimaji wa aina hii ufanyike zaidi ya mara moja kwa mwaka kwani wagonjwa ni wengi wanaohitaji matibabu ya kibingwa ya moyo”