Machinjita: Uchaguzi wa madiwani uliofanyika juzi haukuwa na haki

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 04:35 PM Mar 24 2024
Makamu Mwenyekiti Bara ACT Wazalendo, Isihaka Machinjita.
PICHA: MWANANCHI
Makamu Mwenyekiti Bara ACT Wazalendo, Isihaka Machinjita.

CHAMA cha ACT Wazalendo, kimeeleza kusikitishwa na mwenendo usioridhisha katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mara sita tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021 na kwamba hakuna tofauti na mwaka 2020.

Dukuduku hilo lilitolewa na Makamu Mwenyekiti Bara ACT Wazalendo, Isihaka Machinjita, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi uliofanyika machi 20 mwaka huu.

Amesema uchaguzi huo uliofanyika katika kata 23 haukuwa wa huru na haki akisisitiza katika kata sita ambazo walisimamisha wagombea wake zilifanyika hujuma na kukipatia Chama cha Mapinduzi (CCM) ushindi, na kwamba bila hivyo wangeshinda kakika kata tatu.   

Amesema vitendo vyote vya kiharamia na wizi wa kura vilivyofanyika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 vinaendelea kufanyika kupitia chaguzi za marudio.

“Mapendekezo yaliyoainishwa na Tume ya Haki Jinai yafanyiwe kazi, ili kuvifanyia maboresho vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi katika kusimamia haki za wananchi kwa weledi na usawa.

“Uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopitishwa Februari 2024 kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI uheshimiwe.

“Serikali ipeleke muswada wa marekebisho madogo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuvifanyia mageuzi makubwa vyombo vya haki jinai na mfumo wa uchaguzi kwa ujumla wake” alisema