Askofu Sangu: pokea rushwa lakini usimpigie kura

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 03:59 PM Mar 31 2024
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu.
PICHA: SHINYANGA PRESS
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, amewasihi wananchi wasiwapigie kura viongozi wanaotaka madaraka kwa rushwa, na kwamba wakipewa rushwa wapokee lakini wasipige kura kwa sababu wanaotoa rushwa ni wabinafsi na siyo wazalendo.

Mwaka huu 2024 kuna uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa na Mwakani 2025 kuna uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais.

Askofu Sangu amebainisha hayo leo Machi 31, 2024 kwenye Ibada ya Pasaka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Ngokolo.

"Akikupa rushwa pokea si amekupa, lakini kwenye sanduku hakuna kumpigia kura, kuweni makini sana na watu wanaotafuta madaraka kwa rushwa siyo wazalendo, daima ni wabinafsi tuwe nao macho," amesema Askofu Sangu.

Aidha, amewataka pia Wananchi wale wenye uwezo na sifa ya kuwa viongozi wachukue fomu wagombee kwenye uchaguzi, wakiwamo Wanawake na vijana.

"Akina Mama chukue fomu Mgombea uongozi, Rais wetu ni Mwanamke, Spika wa Bunge Mwanamke na mnauwezo mkubwa wa kuongoza sababu mpo watulivu, pia na vijana tujitokezeeni kugombea kwenye hizi chaguzi," amesema Askofu Sangu.

Pia, amewataka Watanzania kuombea amani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka huu ili upite salama pamoja na kufanyika kwa haki na siyo kuvuruga amani ya nchi.