Askofu Sangu alaani utoaji mimba

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 04:26 PM Mar 31 2024
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu.
PICHA: SHINYANGA PRESS
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewataka wanadamu kuacha kutenda maovu kwa kuendekeza mambo ya giza, ikiwamo na mauaji ya watoto ambao bado hawajazaliwa.

Amebainisha hayo jana kwenye ibada ya mkesha wa Pasaka, iliyofanyikia katika Kanisa la Roman Katoliki Parokia ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.

Amesema Sikukuu ya Pasaka ni kukombolewa kutoka kwenye utumwa wa dhambi, ambapo Yesu Kristo alifia dhambi za wanadamu na kuifungua milango ya mbinguni ambayo ilikuwa imefungwa sababu ya dhambi, na hivyo kuwataka watu kuacha kutenda maovu yakiwamo mauaji ya watoto ambao bado hawajazaliwa (utoaji mimba) bali waishi kwa upendo na amani.

“Tunapo sherehekea Sikukuu hii ya Pasaka tuuvue utu wa kale tuvae utu mpya, wanadamu muacha kutenda maovu ikiwamo uashelati, uzinzi, ushirikina, ugomvi, na mauaji ya watoto ambao bado hawajazaliwa, haya yote ni machukizo ya Mungu ambayo tunapaswa kuyavua,” amesema Askofu Sangu.

“Mnaposherehekea Sikukuu ya Pasaka msherehekee kwa matendo ya nuru na siyo ulevi, mtafuteni Yesu katika neno lake wakumbukeni pia yatima na wajane, mnapowatendea mema mnamtendea Yesu Kristo,” ameongeza.

Katika Ibada hiyo, Askofu Sangu, ameiombea nchi amani pamoja na viongozi wote akiwamo Rais Samia, ili waendelee kuiongoza nchi na kuwaletea watanzania maendeleo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Janeth Magomi, akizungumza kwenye Ibada, amewahakikishia wananchi wa Shinyanga, kwamba kwenye sherehe hiyo ya Pasaka, Jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha Amani inatawala.