Mwinyi: Bidhaa za kimkakati ziondolewe kodi, tozo nchini

By Elizabeth Zaya , Nipashe Jumapili
Published at 02:15 PM Jul 14 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussen Ali Mwinyi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussen Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussen Ali Mwinyi amezitaka mamlaka zinazohusika katika biashara na uwekezaji kwa pande zote za muungano, ziondoe urasimu na kuwezesha zaidi biashara.

Pia amezitaka kupunguza gharama za bidhaa kwa kuondoa kodi na tozo kwenye maeneo na bidhaa za kimkakati.

"Serikali zote mbili zitaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji zaidi katika maeneo ya kimkakati ili kuchangia kikamilifu katika Pato la Taifa na kuboresha mazingira ya biashara ambayo yatanufaisha wananchi wetu.

"Serikali zote mbili zina nia thabiti kuboresha mazingira ya biashara na kwa kuelekeza taasisi za serikali kusomana katika mfumo, kupunguza gharama za bidhaa na kuondoa kodi na tozo kwenye maeneo ya kimkakati," alisema Rais Mwinyi jana mkoani Dar es Salaam.

Rais Mwinyi aliyasema hayo wakati akifunga Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam , maarufu Sabasaba, aliyoyataja ni nyenzo muhimu kwa ukuaji wa biashara nchini.

Pia alizitaka taasisi hizo zenye mamlaka na biashara kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza fedha za kigeni nchini.

Alisema kwa sasa kuna fursa kubwa ya masoko, ikiwamo soko huru la Afrika, soko la Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo wigo wake umeongezeka na kutoa fursa ya kufanya biashara miongoni mwa nchi za Bara la Afrika lenye jumuiya nane na nchi 54.

"Hivyo, TanTrade fanyeni utafiti wa uhakika na uchambuzi wa fursa ziliziko katika masoko hayo ambako bidhaa zetu zinaweza kwenda na kutoa taarifa hizo kwa wafanyabiadhara wetu nchini," aliagiza.

Rais Mwinyi pia alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia vizuri wafanyabiashara wenzao waliowapata (wa ndani na nje) katika maonesho hayo.

Pia aliwataka kuongeza uzalishaji bidhaa ambazo zina mahitaji makubwa katika masoko ya ndani na nje hususani sukari, mafuta ya kupikia, bidhaa za mwani, unga wa ngano, bidhaa za ujenzi, dagaa na samaki.

"Nimefurahishwa na mabadiliko ya maonesho ya mwaka huu, nimeshuhudia hilo katika mabanda nilikopita, kuna kila sababu ya kupongeza mamlaka zilizohusika kuandaa," alisifu Rais Dk. Mwinyi.

Waziri Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaban, alisema wizara yake inayatumia maonesho hayo kama fursa kwa wajasiriamali kutafuta na kutengeneza mtandao wa biashara ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, alisema maonesho ya mwaka huu yana fursa nyingi kwa wafanyabiashara kuunganishwa na wenzao kutoka mataifa mbalimbali, huku zaidi wa kampuni 100 kutoka China zikionesha nia ya kufanya kazi na wafanyabiashara kutoka Tanzania.

"Hii ni jukwaa la vijana kutoka vyuo mbalimbali, hususani vya biashara. Watu wamepata fursa humu, wafanyabiashara wamepata fursa na kushirikiana na wafanyabiashara ndani na nje ya nchi," alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis, alisema mwaka huu maonesho hayo yamevunja rekodi ya miaka 47 iliyopita.

Alisema watembeleaji katika maonesho hayo wameongezeka kutoka 31,000 kwa maonesho yaliyopita hadi 59,000 mwaka huu.

Latifa alisema ukuaji uchumi wa jamii kupitia maonesho hayo ni mauzo ya papo kwa papo ya Sh. bilioni 3.65  ambayo wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa wamenufaika.

"Changamoto za kibiashara zilizotatuliwa katika maonesho hayo ni 396 wakati ajira za muda zilizopatikana ni 21,518.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema, "Zaidi ya nchi 28 zimeshiriki. Hii yote ni kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na serikali, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Biashara (TanTrade)," alisema.