Elimu mikopo kausha damu yashika kasi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:52 AM Jun 09 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa

ELIMU kuhusu mikopo ya fedha kutoka katika taasisi zilizosajiliwa na wananchi kujiepusha na mikopo kutoka taasisi zisizosajiliwa na hatimaye kusababisha maumivu kwa wananchi, maarufu kama kausha damu, imezidi kutolewa kwa wananchi.

Baada ya elimu hiyo kutolewa katika mikoa ya Kagera, Katavi na Geita, sasa imewafikia wananchi wa Kigoma.  

Katika utoaji wa elimu hiyo, wananchi wa wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma, wamepewa ujuzi na maarifa kuhusu mikopo hiyo huku wakitakiwa kuacha tabia ya kukopa fedha kwenye taasisi zisizo na leseni za kutoa huduma za fedha ili kuepuka kuingia kwenye migogoro wakati wa kurejesha mikopo. 

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa, alipokutana na timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo inaendelea na utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika mkoa wa Kigoma.  

Kanali Mallasa alisema wananchi wengi wa Kakonko, wakiwamo watumishi wa umma, wanakabiliwa na changamoto ya kuomba mikopo umiza, maarufu kama kausha damu, kwenye taasisi zisizo rasmi jambo linalosababisha kutapeliwa na kuingia kwenye wimbi la umaskini.

 â€śMikopo hii ya kausha damu kwa kweli imekuwa ikiwaumiza sana wananchi na watumishi wa serikali kutokana na riba kubwa inayowekwa na wakopeshaji pasipo kufuata taratibu za mikopo jambo ambalo halina afya kwa ustawi wa wananchi wetu,” alisema Kanali Mallasa. 

Alisema mikopo inayotolewa mtu akifuatilia hawezi kuona mikataba ambayo hutolewa kwa uwazi bali imejificha na kusababisha wananchi kutoa marejesho makubwa kutokana na riba kubwa, hali ambayo inawaumiza. 

Kanali Mallasa aliwashauri watumishi na wananchi wote kwa ujumla kukopa kwenye taasisi rasmi kwa sababu kuna taratibu zinawekwa na zinafahamika kwa wananchi kwa uwazi. 

Ofisa Usimamizi wa Fedha katika Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, aliwataka wananchi kuwa na utamaduni mzuri wa masuala ya kutafuta na kutumia fedha. 

“Nidhamu ya fedha ni pamoja na kile unachopata katika utendaji wa kazi katika biashara na utumishi kuendana na matumizi. Watu  wengi wamekuwa na matumizi mabaya ya fedha. Anapata  Sh. 10,000 lakini matumizi yake ni 15,000," alisema  Kibakaya. 

Alisema madhara ya kutumia fedha zaidi ya kipato ni kuingia kwenye mikopo ambayo si salama, hivyo ni vyema wananchi kuwa na utaratibu wa kuandaa bajeti ili kile wanachopata kiwekewe utaratibu wa kutumia vizuri. 

Mkazi  wa kijiji cha Kabale wilayani Kakonko, Ernest Mboko, alisema elimu aliyopata imemfanya kuwa na uelewa wa kutafuta fedha, kuweka akiba na kufanya matumizi sahihi kulingana na mahitaji. 

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha inaendelea na utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi katika mikoa mbalimbali ili kuhakikisha wananchi na jamii inapata uelewa na kujifunza namna bora ya matumizi sahihi ya fedha na kujiepusha na matumizi yasiyo rasmi.