SERIKALI ilianzisha mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kuwanufaisha wanachama wanaojiunga nayo kwa manufaa ya baadaye hasa baada ya kufikia umri wa kukoma kufanya kazi. Mifuko hiyo ilikuwa ikitoa mafao mbalimbali kwa wanachama , hivyo kuwawezesha kuishi kwa amani na furaha baada ya kustaafu.
Baada ya kuona kuna mifuko mingi ambayo ilikuwa ikiwahudumia wanachama na baadhi kutofanya kazi kwa ufanisi, serikali iliamua kuiunganisha na kubaki na mifuko mwili tu ambayo ni wa pensheni kwa watumishi wa umma (PSSSF) na ule wa wafanyakazi wa sekta binafsi (NSSF).
Hata kabla ya kuunganishwa na kubaki na hiyo miwili, mifuko hiyo ilikuwa ikivutia makundi mbalimbali wakiwamo wale waliojiajiri ili kujiunga kwa ajili ya kuwasaidia baadaye. Wanachama wa mifuko hiyo walikuwa wanapata mafao mbalimbali kama kiinua mgongo, mazishi, kujitoa, afya na elimu.
Kwa kufanya hivyo, watu mbalimbali kutoka kwenye makundi tofauti walikuwa wakijiunga kwa kulipa kidogo kidogo kila mwezi na hatimaye miongoni mwao walinufaika.
Kutokana na kuwapo kwa mifuko miwili baada ya kuunganishwa, NSSF imeibuka na skimu mpya iliyoboreshwa kwa sekta isiyo rasmi (NISS) kwa lengo la kuwafikia Watanzania wengi zaidi waliojiajiri ili kunufaika na mafao yanayotolewa na mfuko huo.
Akifungua mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, mapema wiki hii jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, alisema skimu hiyo imetengenezwa vizuri na ina faida kubwa kwa jamii. Kwa mujibu wa Waziri Kikwete, skimu hiyo inatoa kinga dhidi ya majanga kama uzee, ulemavu na ugonjwa kwa walengwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema skimu hiyo imeanzishwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi waliojiajiri katika shughuli za kiuchumi huku akiwataja wanufaika na walengwa kuwa ni wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji wadogo wa madini, mama na baba lishe, waendesha bodaboda na wajasiriamali wengine wote.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, ili kunufaika, mwanachama anapaswa kuchangia Sh. 30,000 na atanufaika na fao la matibabu au Sh. 52,200 ambazo atanufaika na matibabu yeye na familia yake. Pia ni rahisi kuchangia kwa kuwa mwanachama anaweza kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki au mwezi kwa kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo atayopewa.
Kwa ujumla, skimu hiyo itakuwa mkombozi kwa wengi kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Toufiq, ambaye pia alipongeza NSSF kwa kuboresha skimu hiyo ambayo itawanufaisha wananchi waliojiajiri kwa kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na mfuko.
Ni vyema sasa makundi yaliyotajwa kuwa ndiyo walengwa yanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ili kunufaika na mafao mbalimbali yakiwamo matibabu kwa siku zijazo. Kama ilivyoelezwa namna ya kujiunga, ni jambo rahisi kwa sababu katika maisha ya kawaida, na ya kila siku, hakuna mtu mwenye dhamira ya dhati ya mafanikio ya baadaye kuwekeza sasa.
Mfumo wa kujiunga na skimu hiyo ni wa udundulizaji na kwa kadri hali ilivyo kwa makundi hayo, kama kuna dhamira ya dhati kutoka moyoni, wengi wana uwezo wa kujiunga kwa manufaa yao ya baadaye. Jambo la kujiuliza ni nani ambaye anaweza kushindwa kundunduliza kila siku, wiki au mwezi ili kunufaika na mfuko huo?
Suala la matibabu, mathalani, limekuwa likiwasumbua wengi hasa wale wasiokuwa na bima ya afya, hivyo ni fursa kwa makundi hayo kujiunga na skimu ya NSSF kwa manufaa yao na familia zao kwa siku zijazo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED