Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Pili wa Utalii wa Vyakula wa Shirika la Utalii Duniani Kanda ya Afrika litakalofanyika kuanzia tarehe 23 hadi 25 Aprili, 2025 Jijini Arusha ambalo linatarajiwa kuwakutanisha wadau zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Duniani ikiwemo viongozi wa ngazi za juu katika sekta ya utalii na ukarimu, watumishi wa serikali, na wataalam wa vyakula.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa pamoja na Sekretarieti ya Shirika la Utalii Duniani Kuhusu Jukwaa la Pili wa Utalii wa Vyakula wa Shirika la Utalii Duniani Kanda Ya Afrika uliofanyika leo Februari 19,2025 jijini Dar es Salaam.
“Tanzania ilichaguliwa kuwa nchi mwenyeji wa jukwaa hilo katika jukwaa la kwanza la Utalii wa Vyakula barani Afrika lililoratibiwa na Shirika la Utalii Duniani Kanda ya Afrika lililofanyika Victoria Falls, Zimbabwe tarehe 26 hadi 28 Julai, 2024. Uamuzi huo ulitokana na ombi la Tanzania kuandaa jukwaa hili nchini kutokana na hazina kubwa ya urithi wa utamaduni na vyakula vya asili kutoka kwa jamii mbalimbali zilizopo hapa nchini” amesisitiza Chana.
Amesema tukio hilo linaandaliwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) pamoja na Basque Culinary Center na linalenga kuangazia uhusiano muhimu kati ya utamaduni wa upishi na utalii na kufanya tathmini ya jukumu muhimu la utalii wa vyakula katika kukuza maendeleo ya kiuchumi, kuhifadhi urithi wa utamaduni na kukuza jamii kiuchumi.
Amefafanua kuwa Mkutano huo utahusisha matukio mbalimbali ikiwemo maonesho ya mapishi ikiwashirikisha wapishi wa mashuhuri na vipaji vya ndani, kuonja aina tofauti za vyakula na vinywaji, mijadala ya jopo na mawasilisho itakayoainisha fursa mpya katika utalii wa vyakula na jinsi unavyoweza kunufaisha uchumi na jumuiya za wenyeji.
Aidha, amesema wahudhuriaji katika jukwaa hilo watapata fursa ya kuungana na kushirikiana katika kubadilishana uzoefu na kujadiliana mikakati na kuongeza ubunifu katika kukuza utalii wa vyakula hivyo ametoa rai kwa wadau wa utalii nchini kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazotokana na tukio hilo ikiwemo kupitia ufadhili wa shughuli mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika, Elcia Grandcourt amesema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa liko tayari kuandaa jukwaa hilo muhimu litakaloleta ladha ya vyakula mbalimbali kutoka katika Kanda ya Afrika na nchi nyingine duniani.
" Tayari nimeshajaribu baadhi ya vyakula vya Kitanzania kama nyama choma na ugali hivyo jukwaa hili litatuwezesha kupata uzoefu ambao Tanzania inayo katika Utalii wa Vyakula" amesema Grandcourt.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED