KUTOKA KWA MTAALUMA MARY NDARO... Uchambuzi wa mwanamama alikosimama kiuchumi

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 08:40 AM Feb 21 2025
 Mtaalamu na mwanaharakati jinsia, Mary Ndaro
Picha: Beatrice Moses
Mtaalamu na mwanaharakati jinsia, Mary Ndaro

HADI sasa ngazi ya dunia, kuna nguvu nyingi kwenye harakati zinazotumika kuwezesha wanawake kuziba pengo la jinsia, kufikia na kunufaika na rasilimali ya taifa.

Kadri nguvu zaidi zinatumika, upande wa pili kuna sauti nyingine ya kuzuka dai, kwamba imeibuka mjadala unaodai ama kumsahau au kupokonywa wanaume uwezo wa umiliki na unufaikaji na rasilimali hizo.

Dai hili, sasa limeibua baadhi ya watetezi wa haki za wanawake kiuchumi, wanaotaka kujua mzizi wa mjadala huo, pia itikadi na takwimu zake.

Hapo ndipo anaibuka mwanaharakati na mtaalam wa maendeleo ya jinsia, Mary Ndaro, anayewasilisha andiko lenye swali ‘Je, Kuwawezesha wanawake kiuchumi kumeathiri uwezo wa wanaume kiuchumi?”

Hapo inaendelezwa na ufafanuzi: “Dhumuni kuu ni kusambaratisha jitihada zinazofanywa na watu wachache, watetezi wa mfumo dume, za kuendeleza ubaguzi ndani ya jamii yetu nakupinga jitihada zinazofanywa na serikali yetu zikiungwa mkono na watetezi wa haki za watoto na wanawake za kuubomoa mfume dume,” anaeleza Mary. 

Mwanamama huyo, anayefanya harakati zake chini ya mwamvuli wa ‘Mtandao wa Wanawake na Katiba,’ anasema ukombozi wa mwanamke kiuchumi ni faida kwa jamii yote, kwa mtoto wa kike na kiume, hasa pale mtoto wa kiume atawezeshwa kutambua kwamba tofauti zao kibaiolojia hazifai kumpunguzia thamani, utu zaidi wa msichana na mwanamke.

DHANA UWEZESHAJI KIUCHUMI

Suala la kumwezesha mwanamke kiuchumi, kunamaanisha kuondoa vikwazo vinavyosababisha wanawake kutofikia, kutumia na hatimaye kunufaika na rasilimali za taifa, ikiwa ni pamoja na rasilimali zitokanazo na jasho la mikono yao.

 Hivyo, anataja dhana ya uwezeshwaji kiuchumi, inahusu kuweka mikakati ya makusudi ya kurekebisha uwiano usio sawia uliosababishwa na mifumo kandamizi, mojawpo ikiwa anautaja ‘mfumo dume’.

 Anaeleza kuwa uchumi ni kigezo kikuu cha kumlinda mwanamke na mtoto wa kike, ikiwamo kulinda utu wake na kumuepusha na vitendo vya ukatili.

Mary anasema kuwa, utafiti unaonyesha mwanamke aliye na uwezo kiuchumi pamoja ná elimu, ana nafasi kubwa ya kuhakikisha watoto wake wanapata elimu iliyo bora. 

Pia, anataja namna tafiti zinavyoonyesha kwamba umasikini wa kipato kwa mwanamke, unaathiri familia nzima na jamii inayomzunguka (kwa mujibu Utafiti wa Umma na Afya- TDHS 2022).

Kinamama wakiwa katika shughuli zao za kiuchumi. Wanatajwa kupitia tafiti, kwamba ngazi yao ya mapato, bado iko chini
Kwenye umiliki wa rasilimali, takwimu hizo za TDHS, zionaonyesha kwamba, asilimia 29 ya wanawake wanamiliki nyumba kwa pamoja (joint) na asilimia saba tu, ndio wanamilikii wenyewe.

“Vile vile asilimia 25 ya wanawake wanamiliki ardhi kwa pamoja na asilimia 8 tu wanamiliki wenyewe.

“Pengo hili linaathiri sana haki na utu wa mwanamke hasa katika kujipatia fursa za kujikwamua kiuchumi,” anaeleza Mary, katika uwasilishaji wake.

Pia, anaieleza kuwa ni hali inayoathiri uwezo wa wanawake kunufaika na huduma za kifedha, kwa vile benki na taasisi nyingi za fedha huwa zinahitaji dhamana, zikiwamo nyumba au ardhi kwa ajili ya kupewa mkopo na mahitaji ya mali zingine za kudumu.

Uchambuzi wake, unaonyesha kwamba asilimia 72 ya wanaume, walikuwa na fursa zaidi za kufaidi fursa za kiuchumi, ikilinganishwa na asilimia 28 tu ya wanawake, kwa mujibu wa marejeo ya kitakwimu.

Hadi kufikia mwaka 2017, kuna asilimia 44 ya wanaume waliokuwa wanamiliki akaunti za pesa, ikilinganishwa na asilimia 33 kwa kinamama, angalizo la mjumuiko unaohusu Benki ya Dunia (World Bank Group: Tanzania Economic update 2022).

Vilevile wanatajwa wanawake wengi, sasa wanakabiliwa na changamoto kwenye biashara, hususani katika kiwango cha kimataifa.

Shida hapo inaelekezwa katika maendeleo kama ya kukosa uelewa wa fursa zilizoko, mahitaji ya soko, kutokufahamu umuhimu wa ongezeko la thamani kwenye mnyororo wa bidhaa (value addition).

Pia, kuna maeneo ya kukosekana fursa za huduma za kifedha, kukosa taaluma ya kuendesha na kumiliki biashara, ukatili kijinsia hasa kwa wanaofanya biashara nje ya Tanzania.

Hata inatajwa katika upatikanaji wa simu za mkononi kuwa jambo muhimu katika ushirikishwaji kifedha, bado ni asilimia 71 pekee ya wanawake, ndio wanamiliki simu za mkononi, ikilinganishwa na asilimia 80 ya wanaume. 

KIPAUMBELE KISEKTA

Hadi sasa, kuna sekta zilizopewa kipaumbele kwenye uwekezaji, hata kutoa ajira kidogo kwa wanawake, mfano wa sekta za usafirishaji, afya ya binadamu na shughuli za kijamií na uchimbaji madini.

Vilevile, takwimu zinawataja wanawake wengi wako katika sekta isiyo rasmi, hata wanaangukia katika ajira hatarishi, huku kukiwapo ujira mdogo, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa kuhusu Jinsia (UN Women gender pay gap brief).

Kunatajwa kuna wanawake asilimia 36.8 walioajiriwa, kama taarifa ya mwaka 2017 inavyoeleza.

Pia, inataja kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi wanaume katika taasisi binafsi, serikali, serikali ya mtaa, ni wanaume.

SEKTA KILIMO

Hadi sasa inatajwa kuwa, kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, huku wanawake wakiwa zaidi ya asilimia 54. 

Licha ya mazingira wezeshi ya kisera na kisheria, bado kilimo kinategemea wakulima wadogo, hususan wanawake, wanaotumia jembe la mkono, mvua na wanaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. 

SEKTA ISIYO RASMI

Katika sekta isiyo rasmi kwenye ujasiriamali, Mary anataja kuwapo asilimia 22 ya nguvu kazi yote nchini.

Hadi sasa Tanzania inatajwa kujishughulisha na sekta isiyo rasmi, ambako asilimia 15 wako vijijini na asilimia 56 mijini. 

Wanawake katika sekta isiyo rasmi ni asilimia 51, ikilinganishwa na asilimia 49 ya wanaume, akirejea ripoti inayowaainisha kinamama, itwayo “Mapping Women Exclusion in Tanzania 2018”.

Pia, kuna umaskini wa muda, unahusisha ukosefu wa muda wa kutosha wa hiari, hasa unaoathiri watu binafsi ambao lazima watoe saa nyingi kwa kazi isiyolipwa, kazi ya ujira mdogo, au majukumu ya ulezi.

Umaskini wa muda, unatajwa kuwa ni suala la kimfumo lililojikita katika kukosekana usawa wa kijinsia.

Hapo inatajwa kuwa, wanawake kwa kiasi kikubwa wanaelemewa na kazi za nyumbani zisizokua na malipo, ikiwamo malezi na kuuguza wagonjwa.

Tafiti zinaonyesha kwamba, wanawake wenye umri kati ya miaka 18 na 19, wanatumia dakika 277(masaa mane na nusu) au zaidi kwa kazi ambazo hazina malipo zisizopewa thamani ya fedha.

Pia, wanaume wanatajwa kutumia dakika 259 (masaa nne na robo) kwa siku kwenye shughuli za uchumi zikipewa thamani ya fedha, ukilinganisha na wanawake wakitumia dakika 155 tu kwenye shughuli za kiuchumi.

Kwa ujumla, inatajwa kuwa wanawake wanatumia saa nyingi zaidi kwa zile shughuli muhimu za kuendeleza binadamu ambazo hazipewi thamani ya fedha, yaani dakika 240 kwa siku wakati wanaume wanatumia dakika 78 tu kwenye shughuli kama hizo. 

Hapo inapewa majumuisho kitaalamu, kuwa ni hali inayoathiri fursa za wanawake kiuchumi na uhuru wa kifedha kwa ujumla.

 “Ni muhimu kutambua kwamba harakati za ukombozi wa wanawake watoto wa kike hazina kusudi wala nia ya kuhamisha ubaguzi kutoka kundi moja kwenda lingine.” anaeleza.

Kuendelea kutumia usawa wa kijinsia kama njia ya kumshusha mtoto wa kiume, ni mitizamo hasi wenye lengo la kurudisha nyuma juhudi za serikali na wadau wengine katika kufikia “ajenda 2030’ inayokusudia kuleta usawa na kuondoa umasikini wa aina zote.

SERA JINSIA

Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023, inabainisha kuwa, mageuzi ya jamii za Kitanzania, sasa inayolenga kuheshimika haki na usawa wa kijinsia kwa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana, wananufaika kwa usawa na fursa zilizopo za kijamii na kiuchumi.

Hapo ndipo yanatajwa kuhitaji msukumo wa kisera na mabadiliko ya fikra na kiutamaduni kwa ngazi zote.

 Aidha, viongozi na jamii nao wanapaswa kuwa na mtazamo unaokubali kukuza na kuendeleza jitihada za kuleta mageuzi katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwezesha maadili chanya, yanayolenga kuimarisha ulinzi na ustawi wa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana wa vizazi vyote katika nyanja zote za maisha.

Inatajwa kwamba, kuimarika kwa haki na usawa wa kiuchumi ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Changamoto za kupatikana haki na usawa kiuchumi zinagusa kasoro kama, kuwapo mgawanyo usio sawa wa kazi katika ngazi ya familia na jamii.

Hapo inatajwa nafasi ya wanawake kubeba uzito mkubwa wa kazi za nyumbani, ikilinganishwa na kiwango cha ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Pia, kuna hali ya kunyimwa haki ya kumiliki rasilimali za uzalishaji, ushiriki na ufikiaji mdogo katika huduma jumuishi za kifedha; na ushiriki mdogo kwenye kazi zenye staha na ujira.

Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo inabainisha kuwa lengo la Kisera ni kuwa na jamii inayoheshimu usawa na haki kwa wote, pia ikaweka Matamko ya sera serikalini, kwa kushirikiana na wadau, yanatajwa ndio yanaiimarisha uwekezaji wenye lengo la kupunguza mzigo wa kazi kwa wanawake na wasichana.

Hapo kuna mambo kama upatikanaji wa huduma za maji, nishati, vituo vya malezi na makuzi ya mtoto.

 Pia, inaelezwa kuwa lengo ni kukuza ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika kazi zenye staha kisekta; rasmi na zisizo rasmi, vilevile inaboresha mifumo na utekelezaji, kukuza upatikanaji na umiliki wa rasilimali za uzalishaji kwa wanawake.

Pia, inapendekezwa suala la kuwekeza kwenye tafiti kuhusu haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake na wanaume na kukuza uzingatiaji wa masuala ya kijinsia katika mipango jumuishi ya uchumi na fedha.