Kigogo Chadema ataka kujibiwa barua ya aliyehoji uhalali wa akina Mnyika

By Enock Charles , Nipashe
Published at 01:27 PM Feb 20 2025
Mwenyekiti wa CHADEMA, mkoa wa Iringa, William Mungai.
PICHA:MTANDAO
Mwenyekiti wa CHADEMA, mkoa wa Iringa, William Mungai.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoa wa Iringa, William Mungai ametaka kujibiwa barua ya kada wa chama hicho, Lembrus Mchome kuhusu uhalali wa uteuzi wa wajumbe wa kamati kuu na viongozi wengine uliofanyika Januari mwaka huu.


Katika maelezo kuhusu barua hiyo aliyoyatoa kada huyo amehoji uhalali wa baadhi ya viongozi wa Chadema akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika  akidai kwamba uteuzi wao haukufuata utaratibu halali wa chama.

Akizungumza na chombo kimojawapo cha habari nchini, Mungai amesema hakuna ubaya kwa chama hicho kumjibu hadharani , Lembrus Mchome kama ambavyo na yeye ameitoa barua yake hadharani ili kuweka mambo sawa ndani ya chama hicho.

 “Kama hatukuogopa uchaguzi kwa vyovyote vile hatuwezi kusema barua ya mtu kutaka ufafanuzi au kupinga hatua fulani ina shida nadhani majibu inabidi yatoke kwa umma kwa sababu na yeye kaitoa hadharani , nafikiri chama kitafanya utaratibu wake na kitamjibu”. Amesema Mungai.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa juu wa viongozi wa chama hicho hali ya mambo bado si shwari licha ya kufanyika jitihada za kuunganisha kambi zilizokuwa zinapingana kati ya ile ya Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa sasa Tundu Lissu.