Makandarasi Arusha, Manyara wahimizwa kumaliza miradi kwa wakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:34 AM Feb 19 2025
Makandarasi Arusha, Manyara wahimizwa kumaliza miradi
 kwa wakati.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makandarasi Arusha, Manyara wahimizwa kumaliza miradi kwa wakati.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi CRB Mhandisi Joseph Nyamhanga, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA) mkoa wa Manyara katika Wilaya ya Babati, Simanjiro na Kiteto, na kampuni ya China Railway Construction Electrification Bereau Group Company Limited (CRCEBG) kukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya umeme.

Amesema hayo tarehe 18 Februari mwaka huu katika ziara ya Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya CRB inayofanywa katika mikoa minne ya kanda ya kaskazini ambayo ni Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa lengo la kukagua kazi za Makandarasi.

Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa hatua ya serikali kusambaza umeme katika kila kitongoji nchini imelenga kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme kwa gharama nafuu.

Aidha msimamizi wa mradi  Mhandisi Michael Masimbani amesema mradi huo umelenga kufikisha huduma ya nishati ya umeme katika kata 139 ambao thamani yake ni zaidi ya shilingi bilioni 21na miongoni mwa wanufaika ni pamoja na kitongoji cha Maisaka ambapo tayari nguzo zimeshasimikwa na nyaya zimeshavutwa na kwamba kilichosalia sasa ni ufungaji wa transfoma. 

Aidha ujumbe huo wa Bodi na Menejimenti CRB umetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa makumbusho ya Hifadhi ya Ngorongoro wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 23 unaotekelezwa na Mkandarasi China Railway 25 Group Ltd katika Wilaya ya Ngorongoro.

Akitoa taarifa kwa wajumbe  hao wa Bodi ya CRB Mjeolojia Ramadhan Khatibu kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro amesema makumbusho hayo yanatarajiwa kukamilika mwezi mei mwaka huu ambapo itaongeza idadi ya watalii watakao tembelea katika hifadhi hiyo. 

Sambamba na hayo Bodi hiyo imetembelea mradi wa upanuzi wa maji wa kilometa 48 unaotoka tenki la maji la Ngorbob jijini Arusha unaotekelezwa na Mkandarasi Jandu Pumblers Ltd katika eneo la Nanja wilaya ya Monduli ambao umelenga kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa wilaya hiyo na vijiji vya jirani.

Pamoja na hayo Mwenyekiti wa Bodi ya CRB Mhandisi Nyamhanga amemtaka Mkandarasi Jandu Plumbers kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa kwa ubora unaotakiwa kwa kuzingatia gharama halisi kwa mujibu wa mikataba yao ili kutimiza azma ya Serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kwa wakati.