Waziri wa Viwanda na Biashara, Seleman Jafo, amewahimiza wananchi wa mkoa wa Njombe kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na miradi ya viwanda inayoendelea kujengwa katika maeneo yao.
Akiwa ziarani mkoani humo, Jafo ametembelea ujenzi wa kiwanda cha mafuta ya parachichi cha Avo Africa kilichopo kijiji cha Mtewele, wilayani Wanging’ombe, pamoja na viwanda vya kuzalisha nondo, saruji, na kuunda magari vinavyojengwa katika kijiji cha Ikelu chini ya Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania Co. Ltd, ambacho kinatarajiwa kutoa ajira 1,000.
“Wananchi wanapaswa kujiandaa na kuchangamkia fursa hii kwa sababu italeta mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Wakinamama waone nafasi ya kupika chakula kwa wafanyakazi, na wakinababa washiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za viwanda hivyo,” amesema Waziri Jafo.
Jafo amesisitiza kuwa kampeni yake ya ujenzi wa viwanda 948 kwa kipindi cha miaka mitano inalenga kuzalisha ajira milioni 6.5, huku ajira za moja kwa moja zikifikia milioni 1.4. Amesema anataka mkoa wa Njombe kuwa mfano wa mafanikio katika sekta ya viwanda.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ameeleza kuwa mkoa huo umejipanga kuhakikisha mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuvutia maendeleo zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Avo Africa, Nagib Karmal, ameishukuru serikali kwa kuwaunga mkono wawekezaji kwa kuwapa uhuru, amani, na usalama, akisisitiza kuwa bila mazingira hayo, maendeleo ya biashara hayawezi kufikiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED