Dk Slaa asota rumande, afikisha siku 41 Keko

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 03:11 PM Feb 20 2025
Mwanasiasa mkongwe, Dk. Wilbroad Slaa.
Picha: Mtandao
Mwanasiasa mkongwe, Dk. Wilbroad Slaa.

Mwanasiasa mkongwe, Dk. Wilbroad Slaa, ameendelea kusota rumande kwa siku 41 katika Gereza la Keko tangu Januari 10, 2025, akikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uongo mtandaoni.

Kusota huko gerezani kwa mwanasiasa huyo ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuwasilisha maombi ya kuzuia dhamana kwa sababu ya usalama wake, kwa sasa kesi imeshindwa kuendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, tayari imeshafika Mahakama ya Rufani.

Pia, hali hiyo ilichangiwa na jopo la mawakili wa Dk Slaa kupeleka maombi ya marejeo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam likiomba ipitie mwenendo wa kesi hiyo kwa madai kuwa haendeshi kwa haki na pia mashtaka anayoshtakiwa nayo ni batili.

Baada ya kutoka kwa uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba kesi hiyo ilirudi Mahakama ya Kisutu iendelee kusikilizwa kwa sababu tayari ilishafikia hatua ya uamuzi na pia ilisema kwamba suala la dhamana ya mshtakiwa lipewe kipaumbele.

Uamuzi huo, DPP hakukubaliana nao ndipo akakata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo, ambapo kwa sasa kinachosubiliwa ni upande wa Jamhuri kukamilisha taratibu za rufaa hiyo.

Mzunguko huo ndiyo uliosababisha hadi leo Dk Slaa hayupo nje kwa dhamana kwa sababu ilipotolewa tarehe ya uamuzi kama mashtaka yanayomkabili ni batili au la upande wa utetezi wakapeleka maombi Mahakama Kuu. Kesi ikishakwenda Mahakama ya juu, Mahakama ya chini haiwezi kuendelea na usikilizwaji.

Leo Dk Slaa alitakiwa kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kesi yake kutajwa, lakini hakuletwa mahakamani licha ya kwamba Mahakama iliagiza afikishwe leo.

Januari 6,2025 Hakimu Mkazi Mkuu Rahim Mushi wa Mahakama hiyo, alitoa agizo kwamba jana (Februari 19,2025) Dk Slaa aletwe mahakamani ili afuatilie kesi yake inavyoendelea, lakini hilo halikuweza kutekelezwa kwa sababu hakuwepo mahakamani.

Hali hiyo ilisababisha Wakili wake, Sanga Melikiole kuhoji mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swalo sababu ya Dk Slaa  kutoletwa mahakamani ikiwa mahakama ilitoa amri ya kuletwa .

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Job Mrema alidai kuwa upande wa Jamhuri hawajapata amri ya kumleta mshtakiwa huyo mahakamani na pia aliieleza Mahakama kwamba kwa asili ya kesi hiyo inaweza kusikilizwa kwa njia ya mtandao "Video Conference".

Hata hivyo, Hakimu aliamuru tarehe ijayo ya kesi hiyo Dk Slaa apelekwe mahakamani. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 4, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Awali, Wakili Mrema aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa huku wakisubiri taratibu za rufani waliyokata kukamilika.

Katika kesi hiyo, Slaa anadaiwa kuwa Januari 9 mwaka huu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisambaza taarifa zanuongo ,kupitia mtandao wa kijamii , wa X zamani  Twitter kupitia jukwaa lililosajiliwa kwa jina la Maria Salungi Tsehai @MariaSTsehai kwa lengo la kupotosha umma.