Mapigano kati ya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) na waasi wa M23 yanaendelea kwa kasi katika mji wa Lubero, uliopo katika Wilaya ya Lubero, mkoa wa Kivu Kaskazini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka uwanja wa vita, mashambulizi bado yanaendelea katika maeneo ya Kitsombiro na Kathondi.
Waasi wa M23 wameishutumu serikali ya Rais Félix Tshisekedi kwa kuwatumia raia kama sehemu ya vita hivyo, wakidai kuwa kuna zoezi la kuwalazimisha vijana kujiunga na jeshi.
Aidha, wanamgambo hao wameendelea kujinasibu kuwa wanakaribia kuuteka mji wa Butembo ndani ya siku chache zijazo. Lubero, mji unaoshikiliwa na FARDC, unatajwa kuwa kitovu cha kiutawala katika wilaya hiyo na upo kwenye nyanda za juu za Kivu Kaskazini.
Katika hatua nyingine, M23 wamevunja ukimya kuhusu suala la nani anayewafadhili silaha, wakidai kuwa vifaa vyote vya kijeshi wanavyotumia vinatoka kwa serikali ya Rais Félix Tshisekedi.
“Hautasikia haya kwenye vichwa vya habari, lakini huu ndio ukweli. Kila mara tunapokamata silaha zao, magari ya kijeshi na kuzuia risasi, zinakuwa mali yetu. Inafurahisha vya kutosha, tunapaswa kuwashukuru FARDC kwa vifaa,” kilieleza chanzo kutoka ndani ya M23.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED