Nusrat Hanje ajipima ubavu kwa Lissu

By Enock Charles , Nipashe
Published at 04:16 PM Feb 21 2025
Nusrat Hanje

MBUNGE wa viti maalum Nusrat Hanje, ameahidi kutoa msaada kwa wasichana wilaya ya Ikungi katika jimbo la Singida Mashariki ili kuwajenga kuwa viongozi bora wa baadae huku akiomba aombewe kutimiza lengo hilo.

Akizungumza na viongozi wa dini wa jimbo hilo, Hanje amesema viongozi wanawake wana wajibu wa kufanya kazi zaidi ili kujenga uaminifu utakaowasaidia wengine kuaminiwa kupewa nafasi za uongozi.

 “Anapopata uongozi mwanamke wajibu wake  hata asipoambiwa ni kwamba ni lazima afanye zaidi ya wajibu wake ili kuhakikisha mabinti wanaaminiwa kwahiyo ni wajibu wangu kufanya zaidi ya wajibu kwa sababu ninawatengenezea njia wanaokuja nyuma yangu” amesema Nusrat.

 “Nina wajibu wa kuhakikisha mabinti zetu ambao wako Unyahati, Isuna na Ikungi Sekondari wanaaminiwa siku moja na wao wakitaka hizo nafasi.” amesema. 

 “Mimi nipo tayari niweke mambo yangu yote kwenye stock (akiba) nishughulike na hili jimbo tu yaani hivi kweli kuna vitu tumeshindwa kuvifanya kitu ambacho mimi sioni kama inashindikana kuvifanya” amesema Nusrat  

 Jimbo la Singida Mashariki limewahi kuongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu tangu mwaka 2010 hadi 2019 na baadaye kuchukuliwa na mbunge Miraji Mtaturu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) hadi sasa.