Naibu Waziri Sangu aipongeza TASAF ujenzi wa Daraja Kitwiru

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:02 PM Feb 21 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Sangu aipongeza TASAF ujenzi wa Daraja Kitwiru.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amepongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Manispaa ya Iringa, kwa utekelezaji na kukamilisha ujenzi wa daraja muhimu katika Kata ya Kitwiru.

Wananchi wa Kitwiru wameeleza kuwa kabla ya daraja hilo kujengwa, walikumbwa na changamoto kubwa hasa wakati wa mvua, ambapo watoto na wakazi walishindwa kuvuka, hali iliyokwamisha shughuli za kiuchumi na elimu.

Wakizungumza baada ya ziara ya Naibu Waziri huyo, wananchi hao wameishukuru TASAF, wakisema daraja hilo limeimarisha mawasiliano na kuwahakikishia usafiri salama hata wakati wa mvua.

Kilichomfurahisha zaidi Naibu Waziri Sangu ni kwamba sehemu kubwa ya vifaa vya ujenzi, kama mchanga, kokoto na mawe, vimenunuliwa kutoka kwa wanufaika wa TASAF waliokuwa wakifanya uzalishaji kupitia vikundi vyao, hatua inayowasaidia kujipatia kipato nje ya ruzuku wanayopokea.