Mume aua mke, mtoto chanzo wivu wa mapenzi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:43 AM Feb 19 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Tanganyika Masele (32), mkazi wa Kisangile, Kata ya Marui, Wilaya ya Kisarawe, kwa tuhuma za mauaji ya mke wake na mtoto wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema tukio hilo limetokea Februari 17, majira ya saa saba mchana, katika Kitongoji cha Buduge, Kata ya Marui, Wilaya ya Kisarawe.

Kwa mujibu wa Kamanda Morcase, waliouawa katika tukio hilo ni Gumba Kulwa (27), mke wa mtuhumiwa, pamoja na mtoto wao, Masele Tanganyika (2).

Ameeleza kuwa Gumba na mwanawe waliuawa kwa kukatwa shingoni kwa kitu chenye ncha kali, kisha miili yao kutupwa pembezoni mwa bwawa la maji lililopo jirani na nyumba yao.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi, ambapo inadaiwa mtuhumiwa alikuwa akitoa vitisho vya kumuua mkewe na mtoto wao mara kwa mara.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza msako kwa kushirikiana na Serikali ya Kijiji pamoja na wananchi, na hatimaye kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

Kwa sasa, mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea kwa hatua zaidi za kisheria.