Bilioni 260/- za CSR Bwawa la Nyerere zilipwe na mkandarasi

Nipashe
Published at 09:47 AM Feb 18 2025
 Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).
Picha:Mpigapicha Wetu
Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

UTEKELEZAJI Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 98.8, Megawatt 1,880 zikizalishwa, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alitoa taarifa hiyo juzi.

Kwa mujibu wa Msigwa, mradi huo wenye thamani ya Sh. trilioni 6.558 na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ulioanza kutekelezwa mwaka 2019, hadi Februari 15, ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 98.8 na mashine nane kati ya tisa zimeshawashwa na kufanya jumla ya megawati 1,880 kuongezeka kwenye Gridi ya Taifa.

Vilevile, Msigwa alisema kuwa tayari mkandarasi ameshalipwa zaidi ya Sh. trilioni 6.5 sawa na asilimia 95.90 ya malipo yote. Kiasi kidogo kilichobaki kimewekwa kwa ajili ya dharura. Kitalipwa baada ya kukakamilika kwa matazamio ya mradi huo.

Nipashe tunapongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia mradi ambao awali ulikumbana na vikwazo kadhaa kiasi cha Umoja wa Mataifa kutaka kuondoa Pori la Akiba Selous kwenye orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia.

Hata hivyo, kuna mambo yenye dosari yanayohusiana na mradi huo yameripotiwa. Mojawapo ni ucheleweshaji utekelezaji miradi ya kijamii (CSR) kwa zaidi ya miaka minne yenye thamani ya Sh. bilioni 262.34.

Wakati mahitaji ya kitaifa ni mengi, hata kuilazimu serikali kukopa, fedha za CSR zimebaki kwa mkandarasi kwa miaka minne. Hii ni hoja iliyoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2022/23.

Katika ripoti hiyo, CAG anabainisha kuwa kifungu cha 2.1.6 cha Makubaliano ya Utekelezaji Miradi ya Kijamii katika utekelezaji mradi huo, kinaelekeza makubaliano ya kina yatajadiliwa na kutiwa saini ndani ya mwezi mmoja baada ya kutiwa saini mkataba wa JNHPP.

Kwa mujibu wa mkataba huo, kama ilivyoripotiwa na CAG, mkandarasi ataanza utekelezaji miradi ya kijamii ndani ya mwezi mmoja baada ya kutia saini makubaliano ya kina huku ikizingatiwa malipo ya awali yamelipwa chini ya mkataba wa mradi wa JNHPP.

Kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji mradi wa JNHPP, miradi ya kijamii itatekelezwa kwa gharama ya Sh. bilioni 262.34 (asilimia nne ya bei ya mkataba). Mkataba wa JNHPP ulitiwa saini tarehe 12 Desemba 2018 na makubaliano ya kina ya miradi ya kijamii yalipaswa kutiwa saini tarehe 13 Januari 2019.

Hata hivyo, hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023, Mkataba wa Kina wa Utekelezaji Miradi ya Kijamii ulikuwa haujatiwa saini, ikiwa ni ucheleweshwaji wa zaidi ya miaka minne (siku 1,610). Kwa mujibu wa CAG, hali hii ilichangiwa na kuchelewa kuanzisha mazungumzo ya kutia saini Mkataba wa Kina juu ya miradi ya kijamii.

Kuchelewa kufikia malengo yaliyokusudiwa kunaashiria hatari ya kushindwa kutekeleza miradi ya kijamii kwa wakati, ikizingatiwa kuwa mradi uko katika hatua ya mwisho za ukamilishaji.

Tarehe 16 Desemba 2019, kama inavyoripotiwa na CAG, kilifanyika kikao cha majadiliano kuhusu utekelezaji miradi ya kijamii. Pande zote zilikubaliana kutekeleza miradi hiyo, hususani ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Dodoma na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Fuga hadi Bwawa la Julius Nyerere.

Hata hivyo, makubaliano haya hayakutiwa saini kutokana na mkandarasi kueleza kuwa miradi iliyopendekezwa haiendani na vigezo vilivyoainishwa katika mkataba wa utekelezaji miradi ya kijamii, kwa kuzingatia aina na utaratibu wa utekelezaji.

Nipashe tunaona kuna haja kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya watendaji wote waliochangia kutotekelezwa matakwa ya kimkataba na kisheria, hata kusababisha zaidi ya Sh. bilioni 260 kutonufaisha wananchi; zikabaki kwa mkandarasi kwa miaka minne.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ndiyo wamiliki wa mradi huo, walipaswa kuwasiliana na Wizara ya Nishati kuhitimisha mvutano kwa kuchagua miradi itakayotekelezwa na mkandarasi.

Pasi na hatua madhubuti kuchukuliwa, kuna hatari mkandarasi akakabidhi mradi wa Bwawa la Julius Nyerere na kuondoka pasi na wananchi kunufaika na Sh. bilioni 262.34 za uwabikaji wake kwa jamii (CSR).