BAADHI ya shule za msingi na sekondari, zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo zinazoweka rehani maisha ya wanafunzi na walimu kutokana na kutumia madarasa na vyoo vibovu.
Mazingira ya aina hiyo, yanazikumbuka hasa shule za vijijini huku baadhi ya wazazi na walezi wakikosa mwamko wa kuhudumia shule hizo ambazo kimsingi ni mali yao. Kwa baadhi ya shule, ni kawaida kukuta madarasa ya miti au yaliyojengwa kwa matofali ya udongo ambayo si imara, hivyo yanaweza kuanguka na kujeruhi hata kuua wanafunzi.
Wakati madarasa yakiwa ya aina hiyo, kwa upande wa vyoo ni vya kienyeji ambavyo navyo si salama kwa wanafunzi. Katika mazingira ya aina hiyo ni wazi kuna haja kuchukua hatua za kuwasaidia wawe salama, maana choo kikititia kinazama na kuwaumiza watoto hata kuwaua.
Mojawapo ya hatua hizo ni bodi na kamati za shule kuwa na mikakati ya kuelimisha na kushirikisha wazazi na walezi katika mipango yote ya maendeleo ya shule ili watambue kuwa wana wajibu wa kuzihudumia. Ninadhani si vyema kusubiri wafadhili kutujengea madarasa, vyoo au kutununulia madawati, badala yake sisi wenyewe tufanye sehemu yetu, hao wafadhili watusaidie katika mambo makubwa
. Sidhani kama wazazi na walezi wakishirikishwa kikamilifu watashindwa kuzihudumia shule kwa kutoa michango yao ya kujenga madarasa au kuchimba vyoo kwa ajili ya watoto wao. Haipendezi kuona wanafunzi wakisomea katika madarasa yanayotishia uhai wao au kujisaidia katika vyoo vibovu huku wazazi na walezi wakiona kama ni jambo la kawaida.
Kwa nini wazazi na walezi wasishirikishwe pale madarasa na vyoo vinapokuwa vibovu na kuambiwa nini kinahitajika ili nao washiriki? Ni vyema bodi na kamati za shule zilione hilo. Yawezekana wapo baadhi ya wazazi na walezi wasiotaka kusikia habari za kuhudumia shule, lakini wakielimishwa, wataelewa na kuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo ya elimu na taaluma ya watoto.
Ninaeleza hivyo kwa sababu kwa sasa kuna mwamko wa wazazi na walezi katika baadhi ya maeneo, wanajenga shule kwa nguvukazi yao pamoja na fedha ili kusogeza elimu karibu na maeneo yao. Kupitia mtindo huo, ninaamini rahisi wakihamasishwa watazihudumia shule badala ya kuziacha zikiwa na madarasa mabovu na vyoo vibovu vinavyohatarisha maisha ya watoto wao na walimu.
Kwanza nielewe kwamba sikatai wafadhili, bali wao watusaidie katika mambo ambayo yako juu ya uwezo wetu, lakini suala la kuchimba na kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo, hayo yako ndani ya uwezo wetu ila kuna sehemu tumekwama. Ninaamini mkwamo unatokana na kutotambua wajibu wetu au kutoshirikishwa.
Hivyo, changamoto hiyo iwe ni fursa ya kutufanya tujue wajibu wetu kuhusu maendeleo ya shule za umma. Miaka ya nyuma kulikuwa na uchakachuaji katika ujenzi wa madarasa na vyoo, lakini serikali imedhibiti hali hiyo, ila ninaamini kuna changamoto ya ukosefu wa madarasa yenye ubora kwa baadhi ya shule za vijijini.
Hali hiyo inatokana na mazingira yenyewe, ingawa huko nako wanafunzi na walimu wanatakiwa kuwa katika mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, hivyo ni vyema wazazi na walezi wakaonyesha mfano wa kutambua umuhimu wa watoto kusomea katika mazingira bora.
Mfano huo ni wao kuwa tayari kushiriki maendeleo ya shule kwa kutumia nguvukazi yao iwe ni kuchimba mashimo ya vyoo, kusomba maji, mawe mchanga ili watoto wawe katika mazingira salama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED