WIKI ya Sheria nchini ilifanyika katika mikoa mbalimbali, kwa ajili ya wananchi kuitambua na kupatiwa elimu ya sheria, jinai na madai.
Wiki hiyo ilianza kwa taasisi mbalimbali za serikali, kutoa elimu kwa wananchi ambao nao watakuwa mabalozi kwa kwenda kuelimisha jamii kwenye maeneo wanayoishi.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wananchi 3,000 wamenufaika na elimu hiyo iliyotolewa na taasisi mbalimbali za sheria, haki, jinai na madai katika wiki hiyo.
Katika viwanja vya Nyerere Square vilivyopo mkoani Dodoma, takwimu hizo zilitolewa na Msajili wa Mahakama ya Tanzania, Eva Nkya, wakati akiyafunga maonyesho hay yaliyofunguliwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Idadi hiyo inaonyesha jamii imepata mwamko wa kufahamu haki zao, hivyo, wananchi hao watakwenda kuwa chachu ya watu kufahamu sheria na namna ya kwenda kudai kwenye vyombo vyenye mamlaka.
Vilevile, wananchi hao watakuwa ni mafanikio makubwa kwa taifa kutokana na kwenda kuwasaidia wenzao kutambua haki zao za kisheria, kuzipata kwa wakati na njia sahihi ya kudai kila siku.
"Nimefarijika sana kuona idadi hiyo imejitokeza kutembelea mabanda ya taasisi za sheria na haki jinai na madai kupata elimu hii yote ni matokeo chanya ya uwepo wa Wiki ya Sheria nchini," alinukuliwa Jaji Nkya, akisema.
Elimu ya sheria ni muhimu kwa jamii kuifahamu kutokana na kwamba inakwenda kusaidia kundi kubwa la wananchi.
Vilevile itawasaidia watoto wadogo kujifunza kutoka kwa wazazi wanao na kuepuka kujiingiza kwenye vitendo viovu ambavyo vimekuwa vikichangia mmonyoko wa maadili.
Vilevile katika kundi la watoto, linaondokana na unyanyasaji pia ukatili, ambavyo vimekuwa vikitokea kwenye maeneo wanayoishi na kufanywa na baadhi ya watu wanaoishi nao.
Vitendo hivyo vitawaepusha na madhara ambayo yamekuwa yakisababisha kupatwa, yakiwemo kuathirika kisaikolojia.
Vilevile watakwenda kuwa mabalozi wazuri wa kukemea vitendo vya rushwa, desturi na mila potofu ambavyo ni kinyume na haki za binadamu.
Wiki hiyo inadhihirisha kwamba, sasa serikali iko mstari wa mbele kukemea ukiukwaji sheria na kuhakikisha watu wake wanaishi kwa amani na utulivu na kutekeleza majukumu yao.
Idara ya Mahakama, Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi za haki jinai zinastahili pongezi kwa kutoa elimu ya katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya mikusanyiko kama shuleni, sokoni na kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Hatua hiyo muhimu kwa sababu inasaidia jamii kufahamu haki zao na kukabiliana na vitendo vya baadhi yao kujichukua sheria mkononi na kusababisha madhara kwa watu wasiokuwa na hatia kuuawa kwa tuhuma mbalimbali.
Serikali inatakiwa kuendelea kutilia mkazo elimu hiyo, ikitolewa kwenye maeneo ya ofisi zake, kuanzia vitongoji, vijiji na kata na kwenye mikusanyiko ya watu.
Kwa kufanya hivyo, matukio mengi ya kutisha kama si kwisha, yatapungua katika jamii.
Mungu Ibariki Tanzania na Watu Wake, amani na utulivu viendelee kuimarika siku hadi siku.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED