Mwalimu wa Madrasa, Mussa Bashiri Mussa, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya kuwafanyia ukatili watoto wawili wenye umri wa miaka 6 na 9, na kuwasababishia madhara.
Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Februari 9, mwaka huu, katika Msikiti wa Sunna uliopo Kiburugwa, Wilaya ya Temeke.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Vicky Mwaikambo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Rabia Ramadhani, akishirikiana na Nicas Kihemba, alieleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo la jinai dhidi ya watoto hao wawili.
Baada ya kusomewa mashtaka, upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Vicky Mwaikambo ameitaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.
Hata hivyo, mshtakiwa amepata dhamana baada ya kukidhi vigezo, ikiwemo barua za utambulisho kutoka Serikali za Mtaa na bondi ya milioni 3 kwa kila mdhamini. Kesi hiyo itatajwa tena Machi 25, mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED