KUVUNJIKA kwa muungano wa serikali nchini Ujerumani, kulifungua njia kwa uchaguzi mpya.
Kansela Olaf Scholz, amepoteza kura ya imani kama ilivyotarajiwa na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Februari 23, mwaka huu.
Kansela mtarajiwa wa Ujerumani Friedrich Merz, ameanza kuonesha nia yake. Anasema anataka kuunda serikali haraka iwezekanavyo, baada ya muungano wa vyama vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union, CSU, kushinda uchaguzi.
Akizungumza mjini Berlin, baada ya kushauriana na wanachama wa vyeo vya juu wa chama cha Christian Democrati Union, CDU, Merz amesema anapanga kuzungumza na mwenyekiti wa chama cha Social Democtaric SPD, kujadili uwezekano wa kuanzisha mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto.
Merz, anayetarajia kuchukua mikoba ya uongozi kutoka kwa kansela anayeondoka Olaf Scholz, amesema pia atawasiliana na Scholz katika siku zijazo kujiandaa kwa kipindi cha mpito cha kukabidhiana madaraka kinachotarajiwa kuchukua wiki kadhaa.
MERZ KUMUALIKA NETANYAHU
Merz, amemwambia Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwamba atamwalika Ujerumani katika hatua inayokaidi waranti wa kukamatwa uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC.
"Kwa kweli tulizungumza kwa simu jana usiku. Alinipigia simu na kunipongeza. Unajua tunafahamiana vizuri na pia nilimwambia tunatakiwa tuonane hivi karibuni baada ya serikali kuundwa.
“Na kama anapanga kuitembelea Ujerumani, pia nilijiahidi tutatafuta njia kumuwezesha aje na aondoke bila kukamatwa. Nafikiri ni wazo la kipuuzi kwamba waziri mkuu wa Israel hawezi kuitembelea jamhuri ya shirikisho la Ujerumani, ataweza kufanya hivyo."
Katika mazungumzo kwa njia ya simu baada ya muungano wa kihafidhina wa vyama vya Christian Democratic Union CDU na Christin Social Union CSU kushinda uchaguzi wa Jumapili iliyopita, Netanyahu amempongeza kansela huyo mteule wa Ujerumani.
Taarifa ya afisi ya waziri mkuu wa Israel, imesema Merz amemwambia Netanyahu kwamba, atamualika aitembelee Ujerumani katika kukaidi uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC kumtaja waziri mkuu huyo kama mhalifu wa kivita.
Msemaji wa chama cha CDU amethibitisha viongozi hao wamezungumza kwa njia ya simu baada ya uchaguzi wa Jumapili, mwishoni mwa wiki, lakini akakataa kutoa maelezo kuhusu mazungumzo yao.
BAERBOCK ATAKA SERIKALI IMARA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, amesema Ulaya iliyo imara na serikali thabiti inahitajika, baada ya chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD, kuongeza maradufu idadi ya kura katika uchaguzi wa mapema uliokamilika Jumapili iliyopita.
Baerbock, mwanachama maarufu wa chama cha Kijani, pia amesema vyama vya kidemokrasia sharti vishirikiane kwa umoja.
Amesema chama cha Kijani kitatafuta kuunga mkono jitihada zozote za serikali ijayo ya Ujerumani, kuzifanyia mageuzi sheria zinazoliwekea kikomo deni la taifa, huku chama hicho kikijiandaa kuchukua nafasi ya upinzani bungeni.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari Baerbock, amesema wanaona wajibu ulio mkubwa kuliko chama chao, utakaokuwa na umuhimu kuamua suala la ikiwa Ujerumani itabaki katika nafasi ya kuweza kuchukua hatua, akigusia mahitaji ya usalama wakati vita vikiendelea nchini Ukraine.
RUSSIA YAIFUATILIA UJERUMANI
Serikali ya Russia, imeelezea matumaini yake kwa uangalifu kuhusu kuimarika mahusiano na Ujerumani.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, amesema anatumai Ujerumani itazingatia hali halisi na ni masuala yapi yatakayokuwa na maslahi na manufaa ya pamoja, lakini wanasubiri jinsi mambo yatakavyokuwa wakati serikali mpya itakapoingia madarakani.
Russia inafuatilia kwa karibu kuona kama Ujerumani chini ya Merz itapeleka makombora yake chapa Taurus nchini Ukraine kutumika kufanyia mashambulizi katika ardhi ya Russia.
CHINA KUSHIRIKIANA NAO
Serikali ya China imesema iko tayari kushirikiana na kansela mpya wa Ujerumani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, amesema China itashirikiana na serikali ijayo ya Ujerumani na inapania kuimarisha mahusiano na mashirikiano ya kimkakati kati ya nchi hizo mbili.
Lin aidha amesema China inaridhishwa na jinsi Ujerumani na Umoja wa Ulaya, wanavyotekeleza jukumu muhimu katika masuala ya kimataifa na inataka kushirikiana na Ujerumani na Umoja wa Ulaya, kuchangia juhudi za amani na maendeleo duniani.
WAFANYABIASHARA WAHIMIZA SERIKALI IUNDWE HARAKA
Wakati haya yakiarifiwa, wajumbe wa biashara wa Ujerumani wamewataka viongozi wa kisiasa waanze mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto haraka iwezekanavyo.
Peter Adrian, rais wa shirika la viwanda na biashara la Ujerumani, DIHK, amesema kutokana na mdororo wa uchumi unaoendelea, suala la muda lina umuhimu mkubwa, huku makampuni yakitumai kutakuwa na muelekeo wa haraka ulio wazi.
Hildegard Müller, rais wa chama cha sekta ya viwanda vya kutengeneza magari, VDA, kundi la ushawishi linaloongoza hapa nchini, amesema Ujerumani inahitaji serikali iliyo imara na thabiti haraka inavyowezekana itakayotatua changamoto kwa umakini na mshikamano na kimkakati.
Wito huu pia umetolewa na shirikisho la viwanda Ujerumani BDI.
Viongozi wa biashara pia wameitaka serikali mpya itakayoundwa ichukue hatua kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu, kupata wafanyakazi wenye ujuzi unaohitajika na pawepo mfumo wa kodi na ushuru unaopendelea na kuleta afueni kwa biashara.
MERZ NI NANI?
Kiongozi wa CDU, Friedrich Merz, ana historia mchanganyiko katika siasa za Ujerumani, kuanzia kumkosoa Angela Merkel, kustaafu na kuingia katika sekta ya biashara, hadi utata wa kukijongelea chama cha siasa kali cha AfD.
Ushindi wake katika uchaguzi huu wa mwishoni mwa wiki, unakamilisha kurejea kwa kushangaza kwa Merz, ambaye alirejea Bundestag mwaka 2021, baada ya kukaa nje ya siasa kwa miaka 12.
Merz mwenye umri wa miaka 69, atakuwa kansela mzee zaidi tangu Konrad Adenauer, kansela wa kwanza wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, ambaye alichukua madaraka mwaka 1949 akiwa na umri wa miaka 73.
Scholz na Merz, wote ni wabobezi wa sheria, lakini kufanana kwao kunaishia hapo.
Merz ni mwanasiasa mrefu wa CDU ni mtu wa haiba ya kuvutia, awe akiingia chumbani au akipanda jukwaani.
Anaonekana kuwa karibu na watu na hata mwenye ucheshi anapozungumza ana kwa ana, ingawa mara nyingine haachi taswira bora anapoinama kuzungumza na watu, jambo analofanya mara kwa mara.
MFANYABIASHARA
Wakati Angela Merkel alipopanda ngazi kuongoza kundi la wabunge wa CDU mwaka 2002 na kuingia ofisi ya kansela mwaka 2005, Merz, ambaye alikuwa na msimamo wa kihafidhina zaidi, alijiondoa na akabaki nje ya siasa kwa miaka mingi.
Akilinganishwa na Merkel, ambaye alionekana kama mwanasiasa mtulivu na mwenye mkakati wa tahadhari, Merz anaonekana kuwa mwanasiasa wa aina tofauti kabisa, akiwa tayari zaidi kuchukua hatari za kisiasa.
Alifanya hivyo hivi karibuni katika mkutano wa mwisho wa chama mwishoni mwa Januari, kabla ya uchaguzi huu, alizua dhoruba ya kisiasa alipojaribu kupitisha muswada mgumu wa uhamiaji bungeni kwa msaada wa chama cha mrengo mkali wa kulia, Alternative for Germany (AfD).
Hatua hii ilisababisha mshtuko kote nchini, huku waandamanaji wakilaani ushirikiano huo kama uvunjaji wa kihistoria wa mwiko wa baada ya vita wa kushirikiana na mrengo mkali wa kulia.
Hata hivyo, Merz aliitetea hatua yake kama kamari iliyolenga kudhoofisha mafanikio ya AfD inayopinga uhamiaji.
Merz, mara nyingi alionekana kama mpinzani wa Merkel mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Mwaka 2001, alijitokeza kuwania ukansela kwa uchaguzi wa shirikisho wa 2002. Hata hivyo, wakati huo, CDU ilimchagua mwanasiasa wa CSU kutoka Bavaria, Edmund Stoiber, ambaye aligombea dhidi ya Kansela wa Social Democrats, Gerhard Schröder na kushindwa.
Merz alijiondoa polepole kutoka kwenye ulingo wa siasa na kurejea katika kazi yake kama mwanasheria.
Baada ya kuondoka siasa, Merz aliingia katika sekta ya biashara, akihudumu katika kampuni za kimataifa za sheria na kuwa mjumbe wa bodi ya kampuni mbalimbali kati ya 2005 na 2021.
Aidha, kati ya 2016 na 2020, aliongoza bodi ya usimamizi ya kampuni kubwa ya uwekezaji BlackRock nchini Ujerumani.amo 2009, hakugombea tena kiti cha Bundestag.
Lakini baada ya Merkel kutangaza kuondoka kwenye siasa mwaka 2021, Merz alirejea na polepole akapanda ngazi tena.
CDU ilimchagua kuwa kiongozi wa chama mnamo 2022 katika jaribio lake la tatu. Alikuwa na sifa ya kuwa mwakilishi wa sera za kiuchumi za kiliberali ndani ya mrengo wa kihafidhina wa CDU.
ASILI YAKE
Merz anatokea Sauerland, eneo lenye milima midogo magharibi mwa Ujerumani na ni mkatoliki pamoja na kuwa mwanasheria, kama baba yake kabla yake.
Hadi leo, anaishi karibu na mahali alipozaliwa. Mwaka 1989, akiwa na umri wa miaka 33, alikuwa mbunge wa Bunge la Ulaya kwa tiketi ya CDU.
Miaka mitano baadaye, alihamia Bundestag na haraka akajipatia sifa kama mzungumzaji mahiri. Kauli zake ndani ya kundi la wabunge wa chama zilikuwa na uzito mkubwa.
MTATA KISHERIA
Merz alipiga kura kupinga kulegezwa kwa sheria za utoaji mimba na dhidi ya uchunguzi wa kijenetiki kabla ya upandikizaji katika miaka ya 1990.
Pia alikumbukwa vibaya kwa kupiga kura dhidi ya kuharamisha ubakaji wa ndoa mnamo 1997.
Daima aliunga mkono nishati ya nyuklia na alishinikiza sera za kiuchumi za kiliberali pamoja na kupunguza urasimu.
Takriban miaka 25 iliyopita, alilalamikia athari za sera ya uhamiaji ya Ujerumani, akazungumzia matatizo na wageni na kusisitiza kuwa lazima kuwe na utamaduni mkuu wa mwongozo nchini Ujerumani.
Tangu kiangazi kilichopita, Merz amejikuta akilazimika kusahihisha na kutetea baadhi ya kauli zake mwenyewe, hususan kuhusiana na uhamiaji na ushirikiano na AfD.
DW
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED