Baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Mwanzo Mgumu, Kata ya Msimbu, Halmashauri ya Kisarawe wamepongeza kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia, wakisema kuwa imewasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zao za kisheria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameeleza kuwa huduma hiyo inapaswa kuwa endelevu, hasa katika maeneo ya vijijini ambako kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu wa sheria.
Sixtus Daniel, mmoja wa wanufaika wa kampeni hiyo, ameishukuru serikali kwa kuanzisha mpango huo huku akitoa wito kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wanaotajwa kuhusika na migogoro katika jamii.
Mratibu wa Msaada wa Kisheria wa Mama Samia Wilaya ya Kisarawe, Robi Happiness, amesema kampeni hiyo inatarajiwa kuwafikia wananchi wa kata kumi ndani ya halmashauri hiyo kwa kipindi cha siku tisa, ambapo watapata msaada wa kisheria bila malipo.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo tayari imeshatekelezwa katika mikoa 19 nchini, huku mkoa wa Pwani ukiwa wa 20. Katika utekelezaji wake, wataalamu wa sheria wanatoa elimu kwa wananchi na kushughulikia migogoro inayowakabili ili kuhakikisha haki inapatikana.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri hiyo, Mwandili Rangi, amewakumbusha wazazi kuwa kushindwa kuwapeleka watoto kliniki ni aina ya ukatili wa watoto, akiwahimiza kuwapa haki hiyo muhimu pamoja na kuwapeleka vituo vya afya wanapokuwa na changamoto za kiafya.
Aidha, amewataka wananchi kuepuka vitendo vya ukatili, kwani vinaweza kusababisha matatizo ya afya ya akili kama vile sonona. Pia amesisitiza kuwa kesi za ukatili zisimaliziwe majumbani, bali zifikishwe kwenye vyombo vya sheria ili haki iweze kutendeka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED