Ujenzi Kituo cha Kupoza Umeme Handeni kuimarisha upatikanaji umeme- Rais Samia 

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:11 PM Feb 25 2025
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Handeni mkoani Tanga utakapokamilika utaboreha upatikanaji wa umeme katika Wilaya za Handeni na Kilindi pamoja na maeneo jirani.

Rais Samia ameyasema hayo leo Februari 25, 2025 katika ziara yake mkoani Tanga wakati akizungumza na wananchi wa Handeni mara baada ya kuzindua Shule ya Wasichana ya Kilindi na Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. 

"Tatizo la umeme hapa Handeni Serikali inalifahamu, imeanza kuchukua hatua kwa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme   kitakachogharimu takribani  shilingi  bilioni 50 za kitanzania ambacho kitaboresha upatikanaji wa umeme." amesema Rais Samia

Ameeleza kuwa,  upatikanaji wa umeme wa uhakika Handeni utasaidia ukuaji wa uchumi pamoja na kuyainua madini ya kinywe ambayo yanapatikana Wilaya ya Kilindi na yanahitaji umeme wa kutosha.

Awali,  Mbunge wa Kilindi, Omari Kigua aliishukuru Serikali  kwa niaba ya wananchi kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 98 kwa ajili ya kutekeleza mradi ya gridi imara utakao husisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkata kupitia Handeni  hadi Kilindi. 

Kigua ameeleza kuwa Wilaya ya Kilindi ina Vijiji 102 ambavyo vyote vimefikiwa na umeme na sasa kazi inayoendelea ni ya kufikisha umeme kwenye Vitongoji.