Wanafunzi 121 UDOM waondolewa masomoni kwa kuchezea mfumo wa matokeo

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 03:19 PM Feb 25 2025
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Picha: Mtandao
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

WANAFUNZI 121 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameondolewa masomoni baada ya kupatikana nah atua ya kuhusika kuchezea mfumo wa matokeo(SR2) Mwaka 2023/24.

Taarifa hiyo imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko UDOM, kufuatia kusambaa mitandaoni taarifa madai ya wanafunzi 400 kufutwa masomo kwa tuhuma za kudukua mfumo.

Kwa mujibu wa Kitengo hicho, wanafunzi 170 walituhumiwa kuchezea mfumo huo na serikali iliunda kikosi kazi kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo na kutoa wito kwa watuhumiwa kufika kusikilizwa kabla ya kutoa maamuzi.

Wanafunzi 148 walisikilizwa, wanafunzi 32 hawakufika kusikilizwa na kati ya waliosikilizwa 121 walikutwa na hatia na  kesi za wanafunzi 15 zinaendelea na uchunguzi zaidi  huku wawili hawakukutwa na hatia.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za Chuo hicho mwanafunzi ambaye hajaridhika na maamuzi ya seneti anapewa nafasi ya kukata rufaa.