Biteko azitaka taasisi za kifedha kuibua walipakodi wapya

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:28 PM Feb 25 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko
Picha: Shaban Njia
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko, amezitaka taasisi za kifedha nchini, kuwaibua walipakodi wapya, kwa kuwawezesha mikopo yenye riba nafuu.

Amesema, ili wakue kiuchumi ifanyike hivyo na sio kuendelea kuwakumbatia matajiri na wafanyabiashara wakubwa pekee.

Biteko ameyasema haya leo, Februari 25, mwaka huu, mjini Kahama, huku akisema mji huoumendeleea kukua kichiumi kila siku, kutokana na uwapo wa shughuli mbalimbali kiuchumi hususani sekta ya kimadini na kilimo.

Amesema, taasisi nyingi za kifedha zimekuwa zikiwajali matajiri na wafanyabiashara wakubwa katika kuwapatia mikopo, ili wazidi kukua kiuchumi na biashara zao na kulisahau kundi la wajasirimali wadogo.

 “Benki hii naomba iwe kimbilio kwa wajasiriamali wadogo ambao wengi wao ni masikini katika kuwaibu kuwa wafanyabiashara wakubwa, ili waje kuwa walipakodi wazuri na ili kuyafanya haya inatakiwa kupatiwa mikopo yenye riba nafuu na sio ile ya kuwaumiza na kuwakatisha tamaa ya biashara,” alisema Dk.Biteko.

Amesema, kwa taarifa alizopata ndani ya miezi sita iliyopita benki hiyo, imeanza kupata faida kwa kipindi kifupi na kutoa sehemu ya faida na kununua vifaa vya matibabu vya thamani ya Sh. milioni 25 na kuvikabidhi katika hospitali ya Manispaa ya Kahama.

Kamishna Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Dk. Charles Mwamwaja, amesema, kuna benki za kifedha 44, matawi 1,000 pamoja na mawakala zaidi ya 100,000 na imesaidia kuwafikia wananchi na kuwahudumia na kuondokana na mikopo umiza.

Amesema, Wizara ya Fedha imendeleea kuchukua hatua juu ya uwapo wa mikopo umiza au chechefu kwa wananchi, kwa kutoa elimu ya fedha, ili kuwajengea uelewa na kutumia fedha kwa usahihi katika malengo waliyokusudiwa na watawafikia mpaka wale waliopo pembezoni.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Jaffari Matundu, akitoa taarifa yake amesema, watawafikia wananchi na kuwahudumia kwa usawa bila ubaguzi wowote na kuhusu kundi la wajasirimali watahakikisha nao linakuwa miongoni mwa wanufaika wa benki hiyo.

Aidha amesema mji wa Kahama unakua kwa kasi hasa kutokana na shughuli za kiuchumi zilizopo na watatoa mikopo mbalimbali yenye riba nafuu, ili kuwaibua walipa kodi wapya na sehemu ya faida huwa wanarejesha kwa jamii, hususani sekta ya afya, elimu na mazingira.