Simulizi undani wa biashara dawa kulevya unavyochafua sekta nchini

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 08:40 AM Jan 17 2025
Mzigo wa dawa za kulevya ulionaswa nchini, ukisafirishwa na jahazi kigeni.
Picha: Mtandao
Mzigo wa dawa za kulevya ulionaswa nchini, ukisafirishwa na jahazi kigeni.

WIKI moja na nusu imepita, Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), ilitoa taarifa ya mzigo mkubwa wa dawa za kulevya, ulioweka rekodi kimataifa, raia wa kigeni na meli yao wakinaswa na sasa wameshafikishwa mahakamani, ikiwa na athari za kiafya, kijamii na mwenendo wa kibiashara nchini. Je undani wa biashara hizo kitaifa na kimataifa ni upi? Fuatilia undani wake kibiashara.

HADI sasa nchini, sera na mwenendo wa kiserikali nchini, ikiwamo dhamira iliyomo katika zama za Awamu ya Sita, ni kuhuisha, pia kupaisha biashara   za haki. 

Na mwenendo wowote ule, katika tafsiri hiyo ya kihistoria, iko katika vita vikali dhidi ya yaliyo haramu, ama kwa mwenendo au aina ya bidhaa husika. Kunakuwapo na mpambano kutoka serikalini kuikabili hali  hiyo.

 Kuna eneo mojawapo, ambalo kitaifa na kimataifa, nchi iko katika vita vikali navyo katika namna endelevu; biashara ya dawa za kulevya, matendo yanayofanyika kitaifa na kimataifa.   

Biashara hiyo, undani wake ni hali inayowahusisha raia wa nchi husika, kwa kushirikiana na magenge ya kihalifu kimataifa, bara Afrika ni sehemu ya waathirika wakuu. 

Wasifu wake ni biashara haramu inayohusisha uzalishaji, usafirishaji, na uuzaji wa dawa za kulevya kama vile heroini, kokaini, bangi na dawa za kemikali kama methamphetamine. 

Biashara huwa haziishi kuvuruga uchumi kitaifa, panakohusika, huku ikichochea ongezeko la uhalifu, kudhoofisha mifumo ya kiusalama, na kuathiri afya na ustawi wa wananchi wake.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODc) Kupitia taarifa yake ya mwaka 2021, inasema, Afrika imekuwa njia kuu ya usafirishaji wa dawa za kulevya kutoka Amerika Kusini na Asia kuelekea Ulaya na Amerika Kaskazini. 

Hiyo inatajwa, kuchangiwa na mambo mbalimbali, ikiwamo udhaifu wa mifumo ya udhibiti, umaskini na ufisadi katika taasisi za umma. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa nchi kama Nigeria, Afrika Kusini, Kenya na Tanzania, zimeorodheshwa kuwa vituo muhimu katika mtandao wa biashara hii haramu.

Mamlaka ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Sheria za Dawa za Kulevya, kupitia ripoti yake ya mwaka 2020, inasema (NDLEA) Nigeria ni moja ya nchi zinazojulikana kwa kiwango kikubwa cha usafirishaji wa dawa za kulevya.

Pia, ripoti hiyo inataja magenge ya kihalifu katika nchi hizo yanahusika kusafirisha dawa za kokeini na heroini kutoka Marekani Kusini na Asia kupitia Afrika Magharibi kwenda Ulaya na Amerika.

Hata hivyo, unatajwa ufisadi kuwapo katika taasisi za serikali na udhaifu wa sheria za kudhibiti dawa za kulevya umechangia kuimarisha biashara hii haramu.

NJIA AFRIKA MASHARIKI

Ripoti hiyo ya UNODC, 2021 inasema nchi za Afrika Mashariki hususani Kenya na Tanzania, zimekuwa njia kuu za kusafirisha heroini kutoka Afghanistan kupitia Bahari ya Hindi.

Inaelezwa kuwa, kuna namna bandari ya Afrika mashariki, kuhusika mara kadhaa katika uvushaji dawa hizi za kulevya.

Hiyo inatajwa, kuhusishwa na mikoa ya ukanda wa Pwani inayotajwa kuwa na kiwango zaidi cha matumizi ya heroini, kuashiria tatizo kubwa la afya ya umma. 

TAARIFA YA NCHINI 

Mnamo siku ya Januari 9, kwa maana ya wiki moja na siku kadhaa zimepita, Kamishna Jenerali mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA),  Aretas Lyimo, akawasilisha taarifa ya udhibiti wa dawa za kulevya ulivyokuwa mwaka jana.

Anasema katika operesheni iliyofanyika mwishoni mwa mwaka uliopita, ulihusisha ukamataji wa kilo 673.2, dawa za methamphetamine na heroin.

Anasema, kati yake 448.3 ziliwahusisha raia wanane kutoka Pakistani katika Bahari ya Hindi, zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi  lenye usajili wa nchi hiyo, ikidaiwa kufanya biashara hiyo kwa miaka 28.

Ni vilevile, kukahusishwa kilo 224.9 zilizokamatwa katika fukwe za bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam.

Ripoti nyingine ya mwaka 2023, inaonesha idadi ya waraibu katika mkoa wa Pwani waliopatiwa tiba katika vitengo vya afya ya akili ilikuwa 62,314.

Hata hivyo, mkoa huo unatajwa kuwa wa pili, kwa kutumia dawa hizo ukiongozwa na Dar es Salaam, ambao ripoti ilionesha kuwapo waraibu 234,317.

Biashara za dawa za kulevya, zinatajwa kuwa na athari kubwa kiusalama kwa mataifa na wananchi wake. 

Ni athari zinatajwa,  zinawezekana kuangaliwa katika nyanja za uhalifu, usalama mipaka, kijamii, na hata siasa.

Mpango wa Kimataifa Dhidi ya Uhalifu wa Kimataifa Ulioandaliwa katika ripoti ya mwaka 2020, umeonesha kuwa biashara ya dawa za kulevya huchochea ongezeko la uhalifu wa kimataifa na ndani.

Aidha, magenge ya wahalifu yanajwa hutumia silaha, kutoa rushwa, na hata kuua, ili kulinda mitandao yao.

Ripoti inafafanua kuwa, katika baadhi ya nchi za Kiafrika, mauaji ya kushukiwa kuwa wahalifu wa dawa za kulevya yameripotiwa mara nyingi. 

Aidha, wizi, ujambazi, na ukatili nao unatajwa kuongezeka katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha matumizi ya dawa za kulevya.

Kuna usalama, kudhoofika kunakotajwa kuumiza mifumo iliyoko, huku ikichangiwa na kuwapo mapato makubwa yanayotokana na biashara ya dawa za kulevya, ili kuwapa nguvu wahalifu kununua ushawishi katika taasisi za kiserikali. 

Hali hiyo inatajwa kusababisha udhaifu wa mifumo ya kiusalama, katika kupambana na uhalifu huu.

Ripoti ya UNODC,2019 inaeleza wazi katika nchi kama Guinea-Bissau, ambayo imekuwa ikiitwa "dola ya dawa za kulevya" kutokana na ushawishi mkubwa wa magenge yake kwenye serikali.

Ripoti ya WHO inasema matumizi ya dawa za kulevya, yanaathiri familia, vijana, na jamii kwa ujumla. 

Vilevile, suala la kuwapo ongezeko la utegemezi wa dawa za kulevya, kunasababisha kuongezeka atatizo ya kiafya, vifo na kuzorota maadili ya kijamii.

Inaelezwa, katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha matumizi ya dawa za kulevya, vijana hukosa dira ya maisha, wakijihusisha na uhalifu au wahanga wa unyanyasaji.

Shirika liitwalo Transparency International, mwaka 2020, likasema biashara ya dawa za kulevya, inachangia kudhoofisha uchumi wa nchi na utulivu wa kisiasa.

Inafafanua kuwa, pesa zinazotokana na biashara hiyo, mara nyingi hazitumiki kwa maendeleo ya kijamii bali kwa kufadhili shughuli za uhalifu au kuficha mali haramu. Pia imekuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa, hasa pale magenge ya wahalifu yanapopata ushawishi wa moja kwa moja katika maamuzi ya kisiasa.

Ripoti ya UNODC (2019), inaeleza kuwa nchi ya Guinea-Bissau imekuwa mfano hai wa nchi inayokumbwa na athari za biashara ya dawa za kulevya. Nchi hii ndogo ya Afrika Magharibi inatajwa kuwa kitovu cha usafirishaji wa kokaini kutoka Amerika Kusini kwenda Ulaya.

Ripoti imeeleza kuwa,Udhaifu wa serikali na ufisadi umeifanya nchi hiyo kushindwa kupambana na magenge ya dawa za kulevya, hali ambayo imeathiri sana maendeleo yake ya kiuchumi na kijamii.

Nayo asasi ya Global Initiative, 2020 katika ripoti yake imeeleza kuwa,Afrika Kusini inakabiliwa na tatizo kubwa la usambazaji na matumizi ya methamphetamine, maarufu kama "tik." 

Miji kama Cape Town imeathirika vibaya, huku magenge ya wahalifu yakitawala mitaa na kushiriki katika biashara hii haramu. 

UNODC,2021 imeeleza katika ripoti kuwa, Kenya na Tanzania zimeathiriwa na biashara ya heroini. Katika maeneo ya Pwani ya Kenya, miji kama Mombasa na Malindi imeripoti viwango vya juu vya matumizi ya heroini, hali inayosababisha madhara ya kiafya na kijamii. 

Tanzania pia inakabiliwa na changamoto za udhibiti wa bandari zake, ambazo zimekuwa njia kuu za usafirishaji wa dawa hizi

Kamishna Lyimo anasema kumekuwepo na vipenyo zaidi ya 600 katika mwambao wa bahari ya Hindi hapa nchini na katika maziwa, hata hivyo serikali imenunua boti maalum kwa ajili ya doria katika ziwa Victoria na kuendeleza mashirikiano na mamlaka nyinginezo pamoja na jamii katika udhibiti na utoaji wa taarifa fiche.

Taarifa ya udhibiti ya mwaka 2024(DCEA)iliyotolewa na Kamishna Lyimo, inaonesha kasi ya udhibiti wa dawa za kulevya Tanzania  inapanda ukilinganisha na miaka ya nyuma .Mwaka 2024 mamlaka hiyo ilikamata kilogramu 2.33 ya dawa za kulevya ukilinganisha na mwaka 2023 ambapo ukamataji ulikuwa kilogramu 1.9.