Pwani wamaliza mnada korosho wakiachiwa mabilioni mkononi

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 04:40 PM Dec 27 2024

Shehena ya korosho, ikishushwa kwenye ghala mkoani Pwani.
PICHA:YASMINE PROTACE.
Shehena ya korosho, ikishushwa kwenye ghala mkoani Pwani.

NI mnada wa nane na wa mwisho wa korosho uliofanyika Kibiti mkoani Pwani, tani 20,150 zimeuzwa kwa kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 60.

Akifunga mnada huo, Meneja wa Chama Cha Ushirika Mkoani Pwani (CORECU), Hamis Mantawela, anasema kuwa ni mnada wa mwisho wa korosho mkoani Pwani. 

"Tumefanya minada nane ya korosho katika mkoa wa Pwani, ambapo mpaka sasa tumefanikiwa kuuza tani 20,150 kwa jumla ya Sh. bilioni 65," anasema. 

Anaongeza kuna wakulima wa zao hilo hawajalipwa pesa zao na kwamba, kama ilivyo minada ya nyuma, kuna wakulima hajalipwa malipo yao, akiitaja kuwa changamoto kwa baadhi yao, huku kukitajwa  taarifa zao za kibenki hazikuwa nzuri. 

Mantawela anasema kwamba, pamoja na changamoto hiyo,wamewaelewesha wakulima utaratibu wa kufanya, ili walipwe haki zao. 

Pia, anataja minada yote imeenda vizuri na wakulima walipata pesa zao kwa wakati,  huku bei ya korosho katika minada ya kwanza; mazao ya daraja la kwanza iliuzwa kwa kilo zaidi ya shilingi 3,000, huku daraja la pili iliuzwa kilo moja kwa bei, zaidi ya shilingi 2000 . 

 " Kadiri minada inapozidi kufanyika, korosho ziliuzwa kwa kilo zaidi ya shilingi 2000," anafafanua Mantawela, akiongeza kuwa bei hizo bado ni bei nzuri, tofauti na bei za miaka ya nyuma. 

Katika hilo, anaipongeza serikali kwa kuandaa mfumo wa uuzaji korosho kwa njia ya mtandao, ambao umeenda vizuri, ikiwamo kufanikisha wanunuzi kujitokeza kwa wingi. 

Pia, anaongeza kuwa maelekezo ya serikali yalitaka wakulima walipwe pesa zao moja kwa moja bila ya kupelekwa katika vyama vya ushirika. 

Anasema, pia kuna kasoro katika malipo ya kibenki, akitaka wakulima walioingiziwa pesa kimakosa kwa mfumo huo wazirudishe. 

"Kuna changamoto imejitokeza ambayo baadhi ya wakulima waliingiziwa pesa mara mbili kimakosa, inatakiwa wazirudishe," anasema. 

Anaongeza kuwa, wamepigiwa simu ili warudishe na wapo waliorudisha, baadhi wakibainika kuwa na elimu duni ya taratibu za kibenki. 

Mwenyekiti wa CORRECU mkoani Pwani Mussa Mng'eresa, anasema huo ni mnada wa mwisho wa korosho katika mkoa huo. 

Anaahidi kwamba, elimu itaendelea kutolewa, ili kuendeleza wakulima wazalishe korosho kwa kiwango, daraja la kwanza. 

Anashauri kama kuna wakulima ambao hawajalipwa, wafuatilie ili walipwe haki zao. Pia, anataja kuwa mbegu za zao la ufuta na mbaazi zitatolewa, kwa wakulima ili waanze kulima mazao hayo 

MZIZI WA UFANISI

Ilikuwa mwaka 2018, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Pwani Evarist Ndikilo, wakati wa uzinduzi wa upandaji wa mikorosho mipya uliofanyika  katika shamba la Ruvu JKT mwanzoni, akatamka:

 “Napenda kutoa rai kwa wakulima wote wa korosho mkoa wa Pwani, kuwa waende katika shamba darasa la Ruvu JKT, kwa ajili ya kujifunza namna ya upandaji wa miche ya korosho ya kisasa.

Akaitaja ni mojawapo ya mazao ya biashara ya kimkakati nchini, ikiwa katika kiwango cha juu kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Pia akasema kuwa, serikali kupitia bodi ya korosho Tanzania, wakati huo ikatoa kilo 7,182 za mbegu bora za korosho kwa mkoa wa Pwani na kuzisambaza katika halmashauri zake zote.

Mbegu hizo zilikadiriwa kuzalisha miche bora 1,039,687 ya korosho, ambayo ikatolewa bure kwa wakulima.

Leo hii, imepita miaka sita, ikiwa katika matarajio ya kuing’arisha Pwani na korosho bora zinazofika sokoni kila msimu, iking’ara kwa daraja la kwanza pale inapotunzwa vizuri.

Ndikilo akawataka viongozi wa wilaya na halmashauri wakati huo, wasimamie vizuri mchakato wa ugawaji wa miche hiyo, na taarifa za wakulima waliokabidhiwa miche hiyo ya korosho zihifadhiwe vizuri kwa ajili ya ufuatiliaji.

Aidha akawataka maofisa ugani wa halmashauri za mkoa huo wa Pwani, watoke maofisini, kwenda kwa wakulima kwa ajili ya kutoa elimu na kanuni za kilimo bora cha korosho.

Wito wake alioutoa wakati huo, bado unabaki kuwa msingi na falsafa katika uzalishaji korosho hadi sasa na aliutamka kuwa: 

 “Ningependa kutumia fursa hii kuwakumbusha na kuwatahadharisha viongozi wa (AMCOS) kubadilika na kama hawatakuwa tayari kubadilika na kusimamia mfumo uliowekwa kulingana na sheria ni afadhali wajivue wenyewe uongozi  na tutawachukulia hatua kali za kisheria.”

Aidha, Ndikilo akawataka wawekezaji wa viwanda kuvijenga vya kubangua korosho na vinavyotengeneza magunia ya kuhifadhi korosho nchini, kuepuka adha ya kuagiza magunia kutoka nje ya nchi.