Ni msako nyumba kwa nyumba kufikisha wenye ulemavu darasani

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:00 AM Feb 04 2025
Baadhi ya watoto wanaohudumiwa na Kaya Foundation.
Picha: Sabato Kasika
Baadhi ya watoto wanaohudumiwa na Kaya Foundation.

KUWATUMIA watu wanaoishi na ulemavu ili kujinufaisha mfano kuwaweka barabarani na bakuli kuomba fedha ni mambo yanayofanyika kwenye miji na majiji mengi.

Inasikitisha kuona wengine wanaungua jua kutwa na baadhi wakinyeshewa na mvua, wakishinda  kutwa wamelowana ili mradi wamewekwa kuwatafutia jamaa zao mapato.

Pamoja na kutumiwa  kuomba fedha barabarani, zipo familia zinazowaficha ndani wakiwaona kuwa ni mkosi, bila kujua kuwa watoto hao wana mchango wa maendeleo kama watapewa maarifa na vipaji vyao kuendelezwa.

Baadhi ya wadau wa watetezi haki za watoto likiwamo Shirika la Kaya Foundation, limeanza kupunguza ukubwa wa tatizo la wenye ulemavu kukosa elimu na huduma muhimu, likiwasaka  na kuwafikisha shuleni.

Kaya imejikita kuwasaka nyumba hadi nyumba na kuwapeleka shuleni kwenye maeneo likifanya kazi hiyo Chamazi, Vingunguti, Segerea na Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Aidha, linawahudumia pia wanawake 20 wenye ulemavu, anasema Annapili Ngome, Mkurugenzi wa Kaya Foundation.
 
 Katika mazungumzo na gazeti hili wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Elimu Duniani jijini Dar es Salaam, Annapili, anasema licha ya jitihada mbalimbali za serikali na wadau kutaka watoto wenye ulemavu wapate elimu, bado kuna kukwama.

Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika 2022 yanataja idadi ya watu wanaoishi na ulemavu kuwa ni  milioni 5.34 karibu sawa na asilimia 11.2 ya Watanzania.

Annapili anataja baadhi ya wazazi walezi wanaowaficha majumbani na kuwakosesha fursa ya kusoma kuwa ni kikwazo.
 
"Shirika letu linajishughulisha na watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum, lilianzishwa mwaka 2023 kwa lengo la kuibua watoto hao kutoka majumbani na kuwapeleka shuleni. Tumekuwa tukishuhudia hali hiyo katika baadhi ya familia," anaongeza.
 
Akielezea jinsi anavyofanya kazi, anasema huwatembelea wananchi wakianzia kwenye ofisi za serikali za mitaa mbalimbali kuelezea lengo lake ili kujua idadi ya watoto aina hiyo katika mtaa ambao hawapelekwi shule.
 
"Kwa njia hiyo tumepata watoto 35 wanaoshi na wazazi na walezi , 15 kati yao sasa wanasoma katika shule mbalimbali za msingi za umma wilayani Temeke na Ilala, na tisa kati yao walianza darasa la kwanza mwaka huu," anasema.
 
Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa wanachokifanya ni kufika katika nyumba zenye watoto walemavu na kutoa elimu kwa wazazi au walezi kuhusu haki za watoto hao ikiwamo kupata elimu.
 
Anasema mlemavu ana haki zote ikiwamo ya kusoma, kulindwa, kutunzwa na kupewa matibabu, kuishi, kuheshimiwa na kutokubaguliwa, kupewa jina, utaifa na kuwafahamu wazazi wake, kutoa mawazo na maoni, kuepushwa na mateso na udhalilishaji na kurithi mali za wazazi wao wapofariki.
 
"Kwa miaka miwili tunajishughulika na watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum, hivyo tuna uzoefu na kile ninachokieleza hasa vitendo vya kuwaficha, kutojua haki zao na kuwatenga," anasema.
 
Hata hivyo, anasema wapo baadhi ya wazazi na walezi ambao hupeleka watoto hao shule na kukataliwa, na kwamba shirika hilo linawaelekeza njia ya kufanya ikiwa ni pamoja na kujua kuwa kuna elimu jumuishi.
 
"Elimu jumuishi inahusisha watoto wasio na ulemavu na wenye ulemavu, hivyo wanapokutana na changamoto ya kukataliwa, tunaingilia kati kuhakikisha wanapokelewa katika shule za umma," anasema.
 
Mkurugenzi huyo anasema, kwa kuwa shirika lake linatoa pia msaada wa kisheria kwa watoto na wanawake na makundi mengine yaliyotengwa kwenye jamii linahakikisha watoto wenye ulemavu wanapata haki zao.
 
Anasema ingawa bado wapo wazazi na walezi wanaowaficha watoto wao wenye ulemavu, wanajitahidi kuwaelimisha watambue kuwa watoto wenye ulemavu wana haki kama wengine wenye viungo kamili.
 
"Sisi tunashughulika na watoto wenye ulemavu karibu wa aina zote na wale ambao wanahitaji miwani, viti mwendo na mahitaji mengine, huwa tunawatafutia kutoka kwa wafadhili wa ndani," anasema.
 
Zunufa Nyasi ni mzazi wa mtoto mwenye ulemavu mwenye miaka tisa ambaye ni miongoni mwa waliohamasishwa kupeleka shule mtoto wake ambaye sasa anasoma Shule ya Msingi Rufu iliyoko Mbande Temeke.
 
Anasema alikata tamaa kumpeleka mtoto shule kutokana na ulemavu wake, lakini shirika hilo lilipomhamasisha ndipo akaamua kumpeleka na sasa anaendelea na shule ingawa kuna changamoto.
 
"Mtoto wangu hawezi kuongea wala kutembea, amepewa kiti mwendo, niliambiwa kuwa ingawa hawezi kuongea, akiwa shuleni kuna kitu anaweza kukipata, hivyo kila ninayempeleka shule anakuwa chini ya uangalizi wa walimu kwenye mazingira ya shule," anasema Zunufa.
 
Zunufa anasema kuwapo kwa mfumo wa elimu jumuishi kunasaidia mtoto wake kuwa katika mazingira ya shule huku yeye mzazi akiendeela na shughuli nyingine za kujitafutia riziki.

Shirika la Maendeleo ya Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linatekeleza kuwa idadi ya watoto wanaoishi na ulemavu duniani ni milioni 240.
 
 Vilevile, ripoti hiyo ya UNICEF ya mwaka 2021 inaeleza kuwa watoto hao wanakosa fursa ikilinganishwa na wenzao wasio na ulemavu katika hatua nyingi za ustawi wa jamii.

Pia mtoto mmoja kati ya 10 anakosa mahitaji ya msingi ikiwamo elimu, ulinzi, chakula na tiba, kwa mujibu wa UNICEF.