MWAKA mpya unapoanza tahadhari za kiafya ni muhimu kuzizingatia na kufahamu cha kufanya ili kujiepusha na magonjwa mbalimbali mojawapo ni tatizo la sasa la afya ya akili.
Wapo wengi wenye changamoto hiyo na mwanzo wa mambo hayo ni matokeo ya athari mbaya kwenye ubongo. Kumbuka kulinda ubongo na kuutunza. BBC inajadili tabia 11 zinaharibu ubongo wako na jinsi ya kuzishinda.
Wiki iliyopita tulizitaja baadhi ya tabia hizo kuwa ni pamoja na kukosa usingizi, kifungua kinywa, kutokunywa maji na kuendekeza msongo wa mawazo.
Leo tunakamilisha ripoti hii kwa kuangalia mienendo ya kila siku inayoumiza ubongo.
KUTUMIA FONI
Vipaza sauti au foni zinazobanwa kichwani au masikioni vina madhara. Wataalamu wanasema kuendelea kutumia vinakudhuru ndani ya dakika 30.
Aidha, kusikiliza kwa sauti kubwa au kwa muda mrefu inamaanisha kelele kubwa hizo zinasababisha kupoteza usikivu.
Pia inahofiwa kwamba kusikia kwako kunapoharibika, hakuwezi kurekebishwa kikamilifu kumbuka kupoteza kusikia huathiri moja kwa moja ubongo.
Kulingana na watafiti wa Marekani, watu wenye upotevu wa kusikia au usikivu hafifu wanakabiliwa na uharibifu wa tishu za ubongo.
Hali hii huongeza hatari ya kupata shida ya kupoteza kumbukumbu na matokeo yake, inakuwa vigumu kusoma na kuzingatia, inasema BBC
Fikiria mara mbili kabla ya kutumia vipaza sauti vya masikioni au kusikiliza wimbo unaoupenda kwa sauti ya juu.
Ikiwa unasikiliza nyimbo kwa kutumia vifaa hivyo au foni masikioni kwa muda mrefu, usiongeze sauti zaidi ya asilimia 60. Pia pumzika kwa saa moja na acha kuvitumia mfululizo.
USIPENDE UPWEKE
Kuwa peke yako kila wakati, kutochangamana na watu, kuzungumza na kupiga hadithi si jambo jema.
Ni muhimu sana kwa afya ya ubongo wako kuzungumza na kuchangamana na watu popote, na kutumia muda mwingi peke yako ni vibaya kwa ubongo wako kama vile kutopata usingizi wa kutosha.
Kuwa na marafiki na kufurahi na familia huiweka akili za binadamu kwenye hali bora kiafya.
Ni kinyume chake kuwa mpweke kwani huongeza hatari ya unyogovu, wasiwasi na shida ya akili.
Ikiwa unataka kuweka ubongo wako kwenye afya, tumia wakati au muda mwingine na marafiki wa karibu na familia mara kwa mara. Ni vyema kuwa na watu wenye mawazo chanya'.
HISIA/MAWAZO HASI
Ikiwa una tabia ya kuwaza fikira hasi au mbaya kila wakati ni kuharibu ubongo. Kwa mfano kuwaza kuwa hakuna kitu kizuri kwako, wala hakiwezi kutokea, unaona dunia ni mbaya sana au huna tumaini kuwa siku zijazo ni giza si jambo jema.
Lakini pia kudhani kuwa huna bahati, ni hatari kwa ubongo. Kwa sababu mawazo mabaya huunda msongo wa mawazo, unyogovu na wasiwasi kwa upande mwingine.
Vile vile, zipo kemikali na vichocheo hujilimbikiza kwenye ubongo ambayo ni sababu kuu ya shida ya akili na kukosa kumbukumbu.
Kwa hiyo, jaribu kuacha mawazo mabaya mara moja. Kufanya hivi mara kwa mara itakuwa tabia inayokuwa na ikiwa huwezi kufanya hivyo peke yako, tafuta msaada wa daktari wa akili.
EPUKA MABAYA
Ili kuwa na ubongo wenye siha kuepuka urafiki mbaya pia ni muhimu sana. Mbali na hilo ni vizuri kujizuia kutazama habari mbaya za vifo, ajali, vurugu mauaji na kupenda sehemu zenye kelele na vurumai.
KWEPA GIZA
Ni hatari kutumia muda mwingi gizani, utafiti nchini Marekani umeonesha kuwa watu ambao hutumia muda mwingi gizani au kutumia muda mrefu katika maeneo yaliyofungwa ambapo hakuna mwanga mwingi na mzunguko wa hewa, mazingira huweka shinikizo sana kwenye ubongo.
Kwa sababu mambo yatokanayo na mwanga wa jua ni muhimu sana kwa ubongo wa binadamu. Vinginevyo, shida kama vile unyogovu zinaweza kutokea iwapo utaishi gizani..
Ili kuweka ubongo wako katika hali ya afya njema, unapaswa kwenda juani kila siku. Nenda nje. Ikiwa uko nyumbani, fungua milango na madirisha.
Pamoja na hayo kupenda kula kupindukia ni hatari kwa ubongo.
Haijalishi jinsi chakula ni 'cha afya' kiasi gani, kula kupita kiasi kunaweza kuharibu ubongo.
Utafiti umeonesha kuwa ulaji kupita kiasi pia huziba mishipa ya ubongo na kupunguza mtiririko wa damu.
Hii inasababisha kupoteza kumbukumbu na kufikiri. Ambayo inaweza kusababisha shida ya akili.
Kula vyakula visivyofaa, vyakula vya kukaanga, vyenye sukari nyingi, vinywaji baridi kutokunywa maji kuna hatari kwa ubongo.
Ndiyo maana ni muhimu sana kuwa na chakula cha wastani na sahihi.
Watu wengi hutumia programu tofauti kufuatilia kalori zao za kila siku. Lakini suluhisho bora ni kutengeneza lishe yako mwenyewe kulingana na ushauri wa mtaalamu wa lishe na uifuate.
Watu wengi wanafikiria kuwa lishe ni juu ya kuondoa mafuta. Lakini kumbuka kwamba asilimia 60 ya ubongo ni mafuta. Kwa hivyo kila aina ya chakula kinapaswa kuliwa.
Lakini inapaswa kuliwa kwa kiasi kinachofaa.
Mbali na hayo, unywaji pombe na uvutaji sigara ni hatari kwa afya. Athari yake mbaya zaidi iko kwenye ubongo.
Mambo haya yanabana mishipa ya fahamu ya ubongo na kuharibu seli.
Kwa hiyo, eneo la ubongo wetu, ambapo kumbukumbu huhifadhiwa, haiwezi kukua.
KOMPYUTA/TV
Muda wa kutumia skrini au kuangalia kioo cha kompyuta au simu una athari kubwa kwa ukuaji wa ubongo. Utumiaji mwingi wa simu za mkononi kwa watoto husababisha uharibifu zaidi kwenye gamba la mbele, ambalo hutofautiana kutoka ujana hadi miaka 25.
Utafiti umeonesha kuwa watoto wanaotumia zaidi ya saa saba kwa siku mbele ya skrini wana gamba jembamba la ubongo.
Kwa sababu kuongea muda mrefu kwenye simu za mkononi kunaweza kusababisha shida kama vile maumivu ya kichwa, kuchanganyikiwa na uvimbe wa ubongo.
Kwa sababu hii, muda wa skrini ya watoto unapaswa kupunguzwa kabisa. Pia, usilale na simu karibu na mwili wako.
Weka simu kwenye begi badala ya mfukoni. Ikiwa unataka kuzungumza kwa muda mrefu, unaweza kuzungumza kupitia spika bila kushikilia simu kwenye sikio lako. Kutuma ujumbe wa maandishi ni bora kuliko kuzungumza.
BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED