ALHAMISI wiki mbili zilizopita, safu hii ilikuwa na sehemu ya kwanza iliyofafanua hali ngumu ya upatikanaji maji wilayani Kilosa, mkoani Morogoro. Endelea nayo, kwa ufafanuzi wa mamlaka zinazosimamia maji na afya, pia hatua zijazo kutatua changamoto hiyo.:
Kuna madai wilayani Msowero, kwamba, hali ya utekelezaji usioridhisha wa Sheria ya Maji ya Mwaka 2019, umesababisha Kata ya Msowero kutoingizwa kwenye Bajeti za Maji katika miaka ya fedha, 2023/24 na 2024/25.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kilosa, Mhandisi Sylvia Ndimbo, anakiri kata ya Msowero yenye vijiji vinne — Msowero, Mambegwa, Mkogwe na Majambaa, bado havijaingizwa kwenye bajeti hiyo za maji.
Uhalisia wake unatajwa kuchangia kuwapo changamoto ya maji kwa zaidi ya miaka 10 mahali hapo, kukiwapo athari mbaya za matukio ya vifo na kulazwa kwa watu 20 kutokana na magonjwa ya matumbo yakiripotiwa katika mwaka 2024.
Mhandisi huyo anasema, kutoingizwa kwenye bajeti, kunasababishwa na ukomo wa bajeti zinazopangwa kila mwaka, ambazo hazitoshelezi kufikia kata na vijiji vyote kwa wakati mmoja.
Mhandisi Sylvia anabainisha kuwa, katika wilaya ya Kilosa yenye vijiji 138, kuna vijiji 23 havina kabisa huduma ya maji safi na salama.
Anataja suluhisho lake, ni kwamba RUWASA ina mpango wa kupeleka maji kwa vijiji hivyo kwa hatua, kwa kuzingatia uwezo wa bajeti ya kila mwaka.
CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU
Mhandisi Ndimbo, anasema RUWASA hufikisha huduma kwenye taasisi za huduma za kijamii, kama zahanati na shule, kulingana na bajeti zilizopo.
Hata hivyo, jukumu la kuingiza maji ndani ya taasisi hizo ni la halmashauri za wilaya.
Mhandisi Sylvia anasema, kwa sasa wanajipanga kutembelea Kata ya Msowero, ili kuwasaidia wakazi wa vijiji na vitongoji vilivyokosa maji, kama A-Mzanini na Sekondari ya Msowero, Kijiji cha Majambaa, kwa kuwachimbia visima vifupi.
Mkurugenzi wa wakati huo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Michael Gwimile, anasisitiza umuhimu wa RUWASA kuanza taratibu za kuweka miundombinu ya maji mara ujenzi wa maeneo yenye miradi ya kijamii unapoanza.
“Hii itasaidia kupunguza changamoto za maji na kuimarisha huduma za kijamii,” anasema Gwimile, akiongeza: “mfano kijiji kuna ujenzi wa zahanati na kama RUWASA wakiweka huduma za maji mapema itasaidia kufikisha huduma hiyo kwa jamii.”
“Pia, hata kama bajeti hazijakaa sawa, watakuwa wamepata huduma na kupunguza malalamiko,” anasema Gwimile.
Anafafanua kuwa, halmashauri nazo hulazimika kuchimba visima vifupi na virefu, baada ya miradi mbalimbali ya kijamii kukamilika, katika baadhi ya maeneo, ili kukabiliana na changamoto za maji.
ATHARI ZAKE
Ofisa Mtendaji Kata ya Msowero, Mustafa Sadi, anasema changamoto za maji zimeathiri wakazi wapatao 30,674 (kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022).
Vijiji kama Mambegwa vina bomba moja pekee, ambalo pia ni bovu, tangu mwaka 2019, taasisi isiyo ya kiserikali ya Waridi, ilisaidia kupunguza changamoto za maji kwa kuchimba visima viwili.
Inatajwa, mafuriko ya mwaka 2024 yalirejesha hali mbaya kwa kusababisha vifo na magonjwa ya matumbo kwa wakazi.
Anavitaja vijiji na vitongoji vilivyokosa maji katika Kata ya Msowero kuwa baadhi ya vitongoji kwenye kijiji cha Msowero, kijiji cha Majambaa, kijiji cha Mkogwe na Mambegwa, ambacho kina bomba moja la Mdundiko, nalo ni bovu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Dk. Selemani Kasuguru, anasema, wagonjwa wa matumbo na kuhara, zaidi inatokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.
Dk. Kasuguru anasema, licha ya idadi ya wagonjwa kushuka kutoka 3,815 mwaka 2022/23 hadi 2,934 mwaka 2023/24, anakiri tatizo bado kubwa.
Hivyo Dk. Kasuguru anahimiza wakazi kutumia dawa za kusafisha maji na kuchemsha maji ya kunywa, ingawa wengi wanaogopa gharama.
Anasema wamekuwa wakiwaelimisha wakazi juu ya matumizi ya dawa za kidonge za kusafisha maji au kuchemsha maji ya kunywa lakini wakazi wengi wamekuwa wakishindwa kufuatilia elimu hiyo, kwa sababu ambazo hazina ukweli ikiwamo kuwa hawana uwezo wa kununua mkaa kwa ajili ya kuchemshia maji ya kunywa.
“Eti wanaogopa gharama, mbona hakuna gharama! Ni rahisi kuchemsha maji na kupata majisafi na salama ya kunywa kwa kila mtu.
“Sababu mtu anaweza kutumia moto uleule anaopikia chakula jioni na baadaye kubandika maji kwenye moto huo na asubuhi yanakuwa yameiva,” anasisitiza daktari huyo wa wilaya.
Dk. Kasuguru anasema, Sheria ya Maji, pia Sera ya Maji ya mwaka 2002 zinahitaji kuimarishwa katika utekelezaji.
Hapo anasisitiza RUWASA inapaswa kuhakikisha mifumo ya usambazaji maji safi na salama inaboreshwa, ili kuzuia magonjwa ya milipuko.
Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limeonya kuwa ongezeko la magonjwa ya kipindupindu duniani, linahitaji hatua za dharura katika upatikanaji maji safi na salama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED