Zaidi ya watu 10 wenye ukoma katika Kitongoji cha Kanoge, Kata ya Misheni, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wamepatiwa msaada wa mbolea kutoka kwa waimbaji wa Kwaya ya Skonge Moravian Gospel.
Lengo la msaada huo ni kuboresha mazao yao na kuwawezesha kupata kipato kupitia kilimo.
Baada ya kukabidhi mbolea hiyo, wanakwaya hao pia walishiriki katika shughuli za kuweka mbolea kwenye mimea ya wakazi hao, ikiwemo mahindi yaliyokuwa yakikosa rutuba na kupoteza ubora wake.
Mwenyekiti wa kwaya hiyo, Richard Masanja, amesema kuwa safari yao hadi Kanoge ililenga kuwasaidia wakazi wa eneo hilo, ambalo lilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1950 kwa ajili ya kuhifadhi na kusaidia wenye ukoma, ili kuongeza tija katika kilimo chao na kuboresha maisha yao kiuchumi.
Kwa upande wao, wakazi wa kitongoji hicho, Kuzenza Masonga na Eva Nasoro, walitoa shukrani zao kwa wanakwaya hao, wakisema kuwa msaada huo utawasaidia kuongeza mavuno tofauti na awali, kwani mazao yao yalikuwa yakiharibika kutokana na uhaba wa rutuba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED