Zimamoto yapania kileleni Ligi Z'bar

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 09:30 AM Feb 10 2025
Eneo la uwanja
Picha: Mtandao
Eneo la uwanja

TIMU ya Zimamoto SC imesema inahitaji kushinda michezo iliyo mbele yake ili kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar

Zimamoto SC ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na alama 31 sawa na Mlandege FC ambao wapo nafasi ya pili wakati kinara wa ligi hiyo Mwembe Makumbi City wenye alama 32.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Zimamoto, Moh’med Ali, alisema azma yake ni kuhakikisha timu hiyo inakaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar.

Alisema ana uhakika wa kutimiza mpango wake huo kutokana na  tofauti ndogo ya alama uliopo kwa timu ambazo zipo katika nafasi nne za juu.

Alisema anaendelea kukifua kikosi chake kwa kuzifanyia maboresho kasoro ambazo zinajitokeza kila mchezo wanaoshuka uwanjani

Aidha, kocha huyo alisema amefanikiwa kwa asilimia kubwa kuliimarisha eneo lake la ushambuliaji hali inayofanya timu hiyo kupachika mabao.

Alisema katika eneo la ushambuliaji wachezaji wamezidisha umakini pamoja na kuzishika mbinu zake nzuri za kiuchezaji hasa wanaposhambulia.

“Sina wasiwasi sana na safu ya yangu ya ushambuliaji, japo nahitaji kuwakumbusha kila tunapokuwa katika uwanja wa mazoezi hasa umakini na kuwa na maamuzi ya haraka,” alisema.

Hata hivyo, alisema kutokana na ubora wa kikosi chake katika mzunguko huu wa lala salama anaamini lengo la kukaa kileleni litatimia.