JUKWAA LA FOCAC: Linavyoakisi utayari wa China kuipa Afrika viwango vingine

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:14 AM Sep 11 2024
Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia jukwaa la Afrika, China  wiki iliyopita.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia jukwaa la Afrika, China wiki iliyopita.

RAIS Samia Suluhu Hassan, ni miongoni mwa marais wanaohutubia Jukwaa la Ushirikiano la China na Afrika (FOCAC), linalomalizika Beijing wiki iliyopita.

Mwalimu wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU), Ning Yi, anazungumzia mkutano huo, akisema kufanyika kwa mara nyingine kwa jukwaa  hilo, kumeleta matokeo chanya ya ushirikiano kwa Afrika.

Ning anasema tangu kuanzishwa kwa FOCAC mwaka 2000 imefanyika mikutano mitatu ya jukwaa hilo ngazi ya juu na minane ya mawaziri ambayo matunda yake ni pamoja na kuongezeka zaidi kwa biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika.

“China imeendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Afrika kwa miaka 15 mfululizo, na katika kipindi hicho, kampuni nyingi zinazotoka katika nchi hiyo, zimechangia ajira zaidi ya 1,000,000 barani Afrika, kwa hiyo haya ni matokeo chanya na ni suala ambalo nchi hizo zinapaswa kujivunia,” anasema Ning.

“Na wakati ushirikiano baina ya China na Afrika ukiendelea kupanuka na kuimarika, mkutano wa viongozi vijana wa pande hizo mikutano mingine kadhaa imefanyika.

Mfano ule wa  ‘think tank’, wa kiraia, wa ushirikiano wa vyombo vya habari, ushirikiano wa kupunguza umaskini na kukuza maendeleo,  wa ushirikiano wa kilimo, wa amani na usalama na majukwaa mengine ya ushirikiano  yameanzishwa  yakiendeleza ushirikiano mwema na  hivi ndivyo vinapaswa kuwa katika kukuza demokrasia na uchumi kwa ushirikiano kwa ajili ya faida kwa pande zote, anasema.

 Aidha anasema FOCAC ina manufaa mengi kama kushauriana kwa uwiano sawa, kuongeza uelewa, kupanua wigo wa maelewano, kuimarisha urafiki na ushirikiano pamoja na kupiga hatua ya maendeleo kwa pande zote kati ya China na Afrika, anaongeza mwalimu huyo.

Anasema huenda baadhi ya washirika hawakulipa nguvu kubwa wakati linaanzishwa lakini kutokana na matunda yanayoonekana sasa tayari kila nchi mshirika anafurahia uwapo wake kwa ajili wa ustawi wa demokrasia na maendeleo.

“Na sasa tunashuhudia jukwaa hili limekuwa kipimo bora cha thamani cha ushirikiano kati ya China na Afrika na limekuwa bendera ya kuongoza ushirikiano wa kina kwa sababu mpaka sasa kuna nchi wanachama wake 55 ambazo zimeanzisha uhusiano wa kidiplomasia, anasema.

Anaongeza kuwa upo umuhimu wa jukwaa hilo kuendelea kuimarishwa na kupewa nguvu zaidi kwa ajili ya ustawi wa kidiplomasia kwa wanachama wake. 

Akihutubia mkutano wa FOCAC, Rais Samia, anasema licha ya changamoto ya uchumi wa dunia miaka ya hivi karibuni, China imeendelea kuwa rafiki wa kweli kwa kuhakikisha utekelezaji wa kiwango cha juu cha makubaliano yaliyofikiwa katika mikutano mbalimbali ya FOCAC.

Anasema jukwaa hilo kwa mwaka huu limekuwa la kihistoria kwa kuwa limefanyika  baada ya muongo mmoja wa kupitishwa na kuzinduliwa kwa Mkakati wa Afrika na China jijini Dar es Salaam na Rais Xi Jinping , alipofanya  ziara  ya kwanza barani Afrika mwaka 2013.

Anasema matokeo ya ushirikiano imara na madhubuti kati ya China na Afrika yanadhihirika kupitia maendeleo makubwa ambayo  Afrika imeyapata kupitia ushirikiano wa nchi hizo pamoja na kufanyika chachu katika kukuza chumi za nchi nyingi za Afrika pamoja na kuleta maendeleo ya watu kupitia miundombinu na ukuaji wa maendeleo ya viwanda vidogo na vikubwa. 

Kadhalika, Rais Samia akishiriki mkutano wa ngazi ya juu kuhusu maendeleo ya viwanda na kilimo cha kisasa akisema licha ya ajenda ya kilimo kuwa ya muda mrefu barani Afrika, lakini kinakosa ukuaji wenye tija, hivyo bara hilo linahitaji kuungwa mkono na nchi zilizoendelea kama China ili kunufaika na kilimo cha kisasa.

Kadhalika anasema  Tanzania imeendelea kuweka mkazo kuendeleza sekta ya kilimo na viwanda na  mchango wa vijana katika sekta hiyo unaongezeka kupitia programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ambayo inalenga kuwanashirikisha katika kilimo chenye tija. 

Rais Samia anasema jitihada za serikali peke yake hazitoshi, akiialika sekta binafsi  ya China kuwekeza Tanzania kwenye mbegu bora, vifaa vya kisasa vya kilimo pamoja na ujenzi skimu za umwagiliaji ili kulima kisasa na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa kilimo. 

Akihutubia wakati akifungua FOCAC Rais wa China, Xi Jinping, anaahidi  kushirikiana na Afrika katika maeneo anuwai ikiwa ni pamoja na kufuta kodi kwa bidhaa zinazotoka  Afrika ambazo tayari zina uhusiano na China.

Rais, Xi Jinping anasema uhusiano wa China na Afrika utazingatia vipaumbele vya maendeleo ili kuhakikisha uchumi jumuishi wa pande hizo za nchi za Afrika inazoshirikiana nazo. 

Ahadi nyingine ni pamoja na utayari wa China kuunga mkono nchi zitakazokuwa wenyeji wa mashindano ya Youth Olympics ya mwaka 2026 na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027.

Anasema  China itawekeza kwenye  afya, ikiwamo ujenzi wa viwanda vya dawa pamoja na kutoa uzoefu katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.