Wananchi wamjengea nyumba mganga

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:38 AM Sep 28 2024
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.
Picha: Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

WANANACHI wa Kijiji cha Ngomai, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma wamempongeza Mganga wa Zahanati yao, Dk. Peter Mwakalosi kwa kumjengea nyumba binafsi kama shukrani ya kutekeleza wajibu wake ipasavyo wa kuwapa huduma bora za afya.

Akisoma risala kwa niaba ya wananchi hao kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule,  Ofisa Mtendaji wa Kijiji hiko, Michael Mwisho, alisema wananchi hao tayari wameshachanga fedha na kumnunulia kiwanja na wameanza kujenga nyumba ya mtumishi huyo.

Alisema mtumishi huyo amejitoa kwao kuisaidia jamii hiyo kutatua changamoto za masuala ya huduma za afya tangu mwaka 2005.

"Tumeonesha nia na upendo wetu kwa Dk. Mwakalosi, hivyo tulimchangia Sh. 4,016,000 na ndipo jamii ilikubaliana inunue kiwanja ili kumkabidhi Dk. Mwakalosi kiwe kiwanja chake binafsi na kilinunuliwa kwa Sh. milioni 3.6 na sasa tunaanza ujenzi," alisema.

Mkuu wa Wilaya hiyo,  Mayeka Simon, aliwapongeza wanachi hao kwa utashi walioonesha wa kuwa na moyo wa shukrani kwa mtumishi huyo.

"Hiki mnachokifanya mmenitia moyo, mmetia moyo na watu wengine, ninyi si wananchi mnaokaa na kusubiri kutoa malalamiko tu. 

"Jambo mlilolifanya ni kubwa sana. Kupitia hiki mlichokifanya Ngomai, mnakwenda kuwa shule kubwa kwa wananchi wengine. Mimi kwenye nyumba ya Peter, nitachangia mifuko 10 ya saruji," alisema.

Akizindua ujenzi wa nyumba hiyo, Mkuu wa Mkoa Senyamule, alimpongeza mtumishi huyo kwa utendaji kazi wake wenye tija kwa jamii hiyo na kwamba watumishi wa serikali wanapaswa kuwaletea furaha wananchi na si kuwa chanzo cha malalamiko.

"Dk. Peter ni mfano wa pekee wa watumishi wanaoajiriwa na serikali, kazi ya watumishi wa serikali wanapoajiriwa ni kuwapa furaha wananchi, lakini baadhi ya watumishi badala ya kuwapa furaha wananchi, wamewapa malalamiko kwa sababu hawatimizi wajibu wao, lakini leo tumeona mfano kwa Dk. Peter," alisema.

"Mimi nimeona ninayo sababu ya kuungana na wanakijiji wa Ngomai kwa kumchangia Dk. Peter, ili dhamira yenu ya kufanya ile nyumba yake ikamilike na apate utulivu akikaa pale ipate kutimia haraka. 

"Nitatoa saruji mifuko 50 lakini kuna mafundi wanahitaji kulipwa, nitatoa Sh. milioni moja," alisema.

Akitoa neno la shukrani, mganga huyo alisema ametumikia zahanati hiyo tangu mwaka 2005 na kuwashukuru wananchi hao kwa kuwa na mioyo ya shukrani.

"Huu ni mwaka wa 19 sasa nipo hapa. Ninamshukuru Mungu sana kwa wananchi hawa kunifanyia hivi, ni jambo ambalo hata mimi moyo wangu wameugusa.

"Ni jambo ambalo hawawezi kukufanyia kama hawajaona ulichokifanya, ukiona unafanya mema unalipwa mema ni kwa sababu wema ni akiba," alisema.