Kigogo CHADEMA aendelea kusota mahabusu gerezani, akosa dhamana

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:28 AM Sep 28 2024
ALIYEKUWA Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu ‘Boni Yai akiteta jambo na wakali wake Peter Kibatala.
Picha:Mtandao
ALIYEKUWA Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu ‘Boni Yai akiteta jambo na wakali wake Peter Kibatala.

ALIYEKUWA Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu ‘Boni Yai’ ameshindwa kupata dhamana baada ya jopo la mawakili wa serikali kuwasilisha maombi mapya na kiapo cha ziada katika kesi ya tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo inayomkabili.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, alitarajia kutoa uamuzi kuhusu maombi ya serikali yaliyowasilishwa Septemba 19 mwaka huu, lakini kabla ya kuutoa, Jamhuri imewasilisha maombi mengine na kiapo cha ziada.

Kutokana na maombi hayo mapya, kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba Mosi mwaka huu, ambapo mahakama itatoa uamuzi wa maombi mawili yaliyowasilishwa na jopo hilo.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha ombi kwamba, mara ya kwanza waliwasilisha kiapo chao katika maombi ya kupinga dhamana ya Jacob kwa njia ya makaratasi, hivyo wanataka wawasilishe kiapo kipya kwa njia ya mfumo ili wakili aione.

Pia waliomba kuondoa ombi moja la mahakama kutoa amri kuingilia mawasiliano katika mtandao wa kijamii wa X unaomilikiwa na Jacob.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Jacob, Peter Kibatala alipinga hoja hizo kuhusiana na kiapo cha ziada kwamba mahakama tayari ilishasikiliza hoja zote na ikapanga tarehe ya uamuzi, hivyo suala hilo haliko sawa kisheria ni suala jipya kabisa.

Pia alidai kuwa kitu wanachofanya upande wa Jamhuri ni kipya katika masuala ya kisheria, kwa hiyo wanapinga ombi hilo kwa sababu halipo kisheria.

Baada ya Hakimu Kiswaga kusikiliza hoja hizo, aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba Mosi mwaka huu atakapotoa uamuzi wa maombi hayo kama yako kisheria au la na pia mahakama itatoa uamuzi wa dhamana ya mshtakiwa.

Katika maombi hao, wanaomba mahakama itoe amri kwa mujibu maombi kuruhusu kupekuliwa akaunti yake ya X na kutoa nywila (password) ili kurahisisha uchunguzi wa akaunti hiyo inayoendana na makosa yake.

Ombi la pili la upande wa mashtaka ni mahakama kutokutoa dhamana kwa mshtakiwa kwa sababu za usalama wake akiwa uraiani.

Katika kosa la kwanza linalomkabili, linahusu kuchapisha taarifa za uongo Septemba 12, mwaka huu. Inadaiwa kuwa Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kwa kupotea kwa wanafamilia wa hizo familia.

Kosa la pili, ambalo lilitokea Septemba 14, mwaka huu linahusiana na kuchapisha taarifa nyingine zinazodaiwa za uongo zinazosomeka 'polisi wanatesa watu na kuua ndio kazi wanayoweza’.