Washtakiwa kesi 'Binti wa Yombo' wamaliza kujitetea

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:23 AM Sep 28 2024
Washtakiwa kesi 'Binti wa  Yombo' wamaliza kujitetea
Picha: Mtandao
Washtakiwa kesi 'Binti wa Yombo' wamaliza kujitetea

WASHTAKIWA wanne katika kesi ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi ya Yombo Dovya, Dar es Saalam, wamemaliza kutoa utetezi wao mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

Walioanza kutoa utetezi wao ni mshtakiwa namba moja, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo na Amin Lema, maarufu Kindamba.

Juzi, washtakiwa wengine wawili ambao ni Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi pamoja na Nickson Jackson, maarufu Machuche, walihitimisha idadi ya washtakiwa wote wanne kutoa utetezi wao mbele ya mahakama hiyo.

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa washtakiwa hao, Meshaki Ngamando, alidai kuwa, "Leo (juzi) tumemaliza idadi ya washtakiwa wote wanne kutoa utetezi wao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Zazibu Mpangule. Kesho (jana) mahakama hiyo itaanza mapitio ya utetezi huo." Washtakiwa hao walikutwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa Jamhuri kuleta jumla ya vielelezo 12 na mashahidi 18 ambao walitoa ushahidi kuhusu kesi inayowakabili washtakiwa hao.

Agosti 19 mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kunyume cha maumbile binti huyo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, iwapo wakithibitika kutenda ukatili huo, watakumbana na adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.