Pinda: Chagueni viongozi waadilifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:45 AM Sep 28 2024

Mbunge wa Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.
Picha:Mtandao
Mbunge wa Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.

MBUNGE wa Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amewaomba wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchagua viongozi waadilifu ambao hawataingiza jamii katika matatizo, yakiwamo ya sekta ya ardhi.

Pinda alitoa rai hiyo wakati wa kikao cha Halmashauri ya CCM kata ya Majimoto, wilaya ya Mlele, mkoani Katavi kilichofanyika jana katika Shule ya Msingi Majimoto.

Aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo namna ambavyo wenyeviti wa mitaa wanavyochangia migogoro ya ardhi, akisisitiza ni jambo lililotokana na kufanyika makosa wakati wa kuwachagua viongozi hao.

"Huko Wizara ya Ardhi, jamani migogoro mingi ni ya wenyeviti kuuza maeneo bila ridhaa ya wananchi.

"Sasa tunaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ombi langu tukawapitishe watu kama mlivyonipitisha mimi na mimi nilivyowapitisha ninyi kwa sifa zenu," alisema Pinda.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, kiongozi bora ni yule aliye tayari kujitolea kwa moyo kufanya kazi kizalendo kwa ajili ya wananchi wote nchini.

Pinda alisema kuwa kutokana na utendaji bora unaofanywa na serikali ya CCM, haoni kama kuna nafasi ya vyama vya upinzani kusimamisha mgombea katika nafasi ya urais.

Pinda yuko katika ziara jimboni kwake ambako mbali na mambo mengine, anatembelea kata zote ndani ya jimbo hilo.