Kituo kikubwa cha Makumbusho kabila la Wanyakyusa kujengwa Rungwe

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 03:14 PM Sep 28 2024
Patrick Mwalunenge akiangalia vifaa vya asili vya kuvulia samaki vilivyotengenezwa na kabila la Wanyakyusa.
Picha:Grace Mwakalinga
Patrick Mwalunenge akiangalia vifaa vya asili vya kuvulia samaki vilivyotengenezwa na kabila la Wanyakyusa.

JAMII ya Wanyakyusa, wanatarajia kujenga kituo kikubwa cha Makumbusho kitachosheni vitu mbalimbali vitakavyoelezea historia ya kabila hilo, mila, desturi na utamaduni.

Akizungumza Septemba 27, 2024 wakati wa kufungua Tamasha la Utamaduni wa Mnyakyusa, linalofanyika kuanzia Septemba 27 hadi 29,  mwaka 2024,  eneo la kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam,  Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, amesema kituo hicho kinatarajiwa kujengwa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Mwalunge amesema Tamasha la Jami ya Wanyakyusa linatoa fursa kujadili na kupeana mbinu za namna ya kujikwamua kiuchumi, kushirikiana katika kuenzi na kudumisha mila na desturi.

“Tamasha hili litukutanisha watu wa jami ya mbalimbali ya kinyakyusa, tunajifunza namna wazee wetu walivyoishi, tunashuhudia ngoma na vyakula vya asili vya kabila letu, hapa ni sehemu inayotuunganisha na wenzetu kutoka maeneo mbalimbali,” amesema Mwalunenge.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Enelen Mwakapila, amesema nyumba za asili za kabila hilo, mavazi ya asili, chakula na warsha za namna ya kuenzi utamaduni na kujikwamua kiuchumi.

Amesema licha kufanikisha tamasha hilo, lakini hawana chombo cha kitaifa cha kusimamia maudhui, kupeana elimu  kuhusu utamaduni wa Mnyakyusa, kupungua kwa vijana wanaohamasisha kulinda na kuuenzi utamaduni wao.

Kaimu Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa, Frida Kombe, amesema wataendelea kushirikiana na Jamii ya Wanyakyusa katika kudumisha mila, desturi na utamaduni wao.

Amesema majukumu waliyonayo ni kutafiti, kuhifadhi na kuelimisha jamii kuhusu urithi wa utamaduni wa asili wa nchi  ambao unapatikana kwenye vituo saba vya makumbusho yakiwemo na maeneo 163 ya Malikale.

“ Makumbusho ya Taifa ni Taasisi yenye jukumu kukuza na kuendeldeza utamaduni wa makabila yote nchini, tuna simamia program mbalimbali kama vile siku ya utamaduni wa mtanzania ambayo inaratibiwa na Kijiji cha Makumbusho  ikiwamo jamii ya Wanyakyusa ambayo leo wanaisheherekea,” amesema Kombe.

Mwenyekiti wa machifu kutoka Wilaya ya Kyela mkoani  Mbeya,    Uswege Mwakabulufu amesema, Tamasha hilo litasaidia kuondoa dhana potofu ya kudhaniwa   machifu ni wachawi.

Amesema kitendo hicho sio cha kweli na  jamii inapaswa kuachana na dhana potofu, akatolea mfano kwamba Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amewapata thamani machifu kwa kuamua kushirikiana nao kwenye shughuli mbalimbali ikiwemo kulinda na kuenzi mila na desturi za nchi.

Amesema Rais. Dk. Samia amefanya hivyo kwa sababu ametambua mchango wa machifu nchini kwamba ni watu wanaolisaidia Taifa katika kukabiliana na masuala mbalimbali yanayokwenda kinyume na maadili.