Mwanakijiji apigwa risasi na askari msako dawa za kulevya

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 07:36 AM Sep 28 2024
Bastola.
Picha:Mtandao
Bastola.

MKAZI wa kijiji cha Tumuli, wilayani Mkalama, mkoani Singida, Hamis Salumu (40) amelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Benjamini Mkapa, mkoani Dodoma baada ya kupigwa risasi na askari na kumjeruhi miguu yote miwili.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Mayunga Mayunga, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema mwananchi huyo alipigwa risasi Septemba 18, 2024 baada ya askari kufika nyumbani kwake kufanya upekuzi wa dawa za kulevya.

Alisema askari walipofika nyumbani kwa Salumu kufanya upekuzi, hawakumkuta na baada ya dakika chache, mtuhumiwa alifika kwake akiwa na vijana sita wakiwa na silaha za jadi zikijumuisha mapanga huku wakipiga kelele zilizoashiria kuzuia askari kufanya upekuzi.

Kamanda Mayunga alisema kuwa baadaye idadi ya watu iliongezeka na kufikia 20 ambapo Salumu na wenzake walianza kumkimbiza askari aliyekuwa na bunduki kwa nia ya kumdhuru huku wakitaka kuchoma moto gari la serikali lililokuwa linatumika katika operesheni hiyo.

Alidai kuwa kutokana na hali hiyo, askari walilazimika kufyatua risasi hewani kwa lengo la kuwaonya wasiendelee na dhamira yao ya kumshambulia na kuchoma moto gari la serikali, lakini walikaidi na ndipo wakampiga risasi Hamis Omari Salum, ikimjeruhi miguu yote miwili.

"Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Ludani Prosper na Hamis Omar ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Benjamini Mkapa, mkoani Dodoma," alisema.

Kamanda Mayunga alisema wanawashikilia pia watu watatu kwa uchunguzi wa tuhuma za mauaji ya Athuman Kikalanga (37), mkazi wa kitongoji cha Mapinduzi, kijiji cha Usure, wilayani Iramba.

Waliokamatwa ni Juma Mitigo, Juma Kikalanga na John Songelaeli huku chanzo cha mauaji hayo kikidaiwa kuwa ugomvi wa kifamilia kati ya Juma Kikalanga na Athuman (marehemu) kuhusu mgawo wa mali iliyoachwa na marehemu baba yao.

Alisema mtu huyo aliuawa kwa kupigwa risasi kwa kutumia bunduki aina ya Shotgun Septemba 19, 2024 saa nne usiku wakati akirudi nyumbani kwake akitokea kwenye matembezi yake ya kawaida.

Kamanda Mayunga alisema uchunguzi wa awali wa tukio hilo umebaini kuwa Athuman alipigwa risasi na Juma Mitigo (45), maarufu Kandugu, mkazi wa kijiji cha Usure kwa kutumia bunduki aina ya shotgun aliyopewa ba Juma Kikalanga (47).

Alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo (Juma Kikalanga) alipata bunduki kutoka kwa John Kalanda (51), mkazi wa kitongoji cha Kabutwa, kijiji cha Luzilukulu ambaye ni mmiliki halali wa bunduki hiyo.

Kaimu Kamanda Mayunga alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio hayo na ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

"Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, watii sheria bila shuruti na kuachana na biashara haramu ikiwamo ya dawa za kulevya," alisema.