Wamwangukia Rais kitongoji chao kufutwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:09 AM Sep 28 2024
 Rais Samia Suluhu Hassan
Picha:Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan

WAKAZI wa Kitongoji cha Sengerema, kijiji cha Mwendakulima, kata ya Butengoruma, wilayani Chato, mkoani hapa wamelalamikia hatua ya serikali ya kufuta kitongoji hicho na kuondoa kituo cha kupiga kura za serikali za mitaa.

Kutokana na uamuzi huo, wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kurejeshwa ili kupata kituo cha kupigia kura na kuchagua viongozi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi hao, akiwamo Petrol Katemi, walisema katika uchaguzi uliopita, walikuwa wanapigia kura katika kitongoji hicho, lakini kwa sasa hawajui kituo watakachopigia kura.

"Tunamwomba Rais Samia ufike utusaidie ili kitongoji chetu tupate kituo cha kupigia kura na hakuna maelezo yoyote ya kituo hiki kuondolewa katika vitongoji vilivyopo hapa," alisisitiza Katemi.

Mwananchi mwingine Vicenti Matongo, alisema kitendo cha kitongoji hicho kufutwa na kutowekewa kituo cha kupiga kura, ni kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupiga kura na kuchagua kiongozi wao wanaowataka.

Mkazi mwingine wa kitongoji hicho, Philipo Magesa, alisema wamekuwa kitongojini huko tangu mwaka 1985, wakishiriki upigaji kura katika eneo hilo na kuchagua viongozi wao wanaowataka kama kawaida, lakini sasa wamekumbwa na taharuki baada ya kuambiwa kuwa kimefutwa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mwendakulima, Kata ya Iparamasa, wilayani hapa, Andrew Nkomeji, alikiri kuwapo sintofahamu hiyo baada ya kitongoji hicho kudaiwa kufutwa.

"Kijiji hiki kina vitongoji vinne, lakini hati ya kijiji katika orodha imeanisha vitongoji vitatu; Idosero, Mwendakulima A na Mwendakulima B. Kwenye orodha ya Uchaguzi wa Serikali, kitongoji cha Sengerema hakipo," alisema Andrew.

Kuhusu malalamiko ya wananchi hao, alisema kuwa miaka iliyopita walikuwa wakipigia kura huko na hivyo kuomba mamlaka na vyombo husika kurejesha hati ya kijiji cha Mwendakulima ili kuainisha mipaka ya maeneo hayo.

"Hiki kitongoji kina wakazi 624 na kaya zaidi ya 156 ambazo zinaweza kupoteza haki ya kupiga kura kutokana na sintofahamu hii," alisema Andrew.   

Nipashe ilipomtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mandia Kihiyo, ili kupata ufafanuzi wa sintofahamu hiyo, simu yake iliita pasi na kupokewa.

Kilio hicho kinakuja kutokana na taarifa ya ratiba ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.

Taarifa yake ilitaja siku ya kuchukua fomu za wagombea na siku rasmi ya uchaguzi kuwa ni Novemba 27 mwaka huu.