DFC, Citi watangaza mkopo mpya Dola milioni 320 CRDB

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:53 AM Sep 28 2024
DFC, Citi watangaza mkopo  mpya Dola milioni 320 CRDB
Picha:Mtandao
DFC, Citi watangaza mkopo mpya Dola milioni 320 CRDB

SHIRIKA la Fedha la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (DFC) na Citi wametangaza ufadhili wa Dola za Kimarekani milioni 320 kwa Benki ya CRDB.

Ufadhili huo umelenga kuimarisha uwezo wa benki hiyo kutoa mikopo kwa biashara ndogo, hasa zinazomilikiwa na kuongozwa na wanawake.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa DFC, Nisha Biswal, aliungana na Mkuu wa Kitengo cha Fedha za Wakala wa Biashara za Nje wa Citi, Richard Hodder na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika hafla ya kutia saini makubaliano hayo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na ujumbe wa maofisa wakuu wa serikali walihudhuria hafla hiyo kushuhudia utiaji saini huo.

Mradi huo utasaidia zaidi ya biashara ndogo 4,500 Tanzania, moja ya masoko yenye nguvu zaidi barani Afrika.

Dola milioni 60 zitaelekezwa kusaidia biashara ndogo zinazomilikiwa na kuongozwa na wanawake zitakazokidhi vigezo vya kujumuishwa katika Mpango wa Kuwasaidia Wanawake wa DFC 2X, ili kusaidia kushughulikia changamoto za kiuchumi zinazowakabili wanawake duniani kote.

Dola milioni 25 zitatolewa pia kusaidia biashara ndogo Burundi.

Mkopo huo unadhihirisha dhamira ya dhati ya DFC ya kupanua ushirikiano wake Tanzania na kuimarisha ushirikiano wake wa sasa na kuchunguza fursa mpya za ushirikiano, kukuza usalama wa kiuchumi katika kanda na kote barani Afrika.

"DFC imedhamiria kwa dhati kusaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania, ikilenga kuwezesha uwekezaji ambao utakuwa na manufaa makubwa zaidi kwa watu na jamii," alisema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa DFC Biswal.

Alisema mkopo huo utaunga mkono utoaji mikopo kwa maelfu ya biashara ndogo zinazopambana kusukuma gurudumu la maendeleo ya kiuchumi nchini kote.

"Mkopo huu wa Dola milioni 320 utaongeza upatikanaji fedha kwa biashara ndogo za kati, zinazoendeshwa na kusimamiwa na vijana na wanawake Tanzania na Burundi, ukiwajengea uwezo wajasiriamali hawa kuanzisha na kuendesha biashara zenye ubunifu na kujenga ukuaji endelevu.

"Tuna uhakika kuwa ufadhili huo hautapanua tu biashara bali pia utaimarisha usawa wa kijinsia, kuwapa wanawake wajasiriamali msaada wanaohitaji ili kufanikiwa na kuchangia maendeleo jumuishi ya uchumi," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Nsekela.

Alisema fedha hizo kutoka DFC na Citibank zitaimarisha juhudi za Benki ya CRDB katika kukuza ukuaji uchumi jumuishi katika kanda, kama sehemu ya mpango wake wa kimkakati wa miaka mitano unaolenga kuongeza msaada kwa wajasiriamali.

Alibainisha kuwa pamoja na bidhaa bunifu za kifedha, benki hiyo kupitia wakala wake, CRDB Bank Foundation imeweka msisitizo mkubwa kwenye ujenzi wa uwezo kwa wajasiriamali vijana na wanawake kupitia mafunzo ya uelewa wa kifedha na ujasiriamali. Nsekela alisema ushirikiano huo na DFC na Citi utaongeza kasi zaidi ya juhudi hizo.

"Citi inafanya kazi kutekeleza ajenda yetu ya fedha za kijamii kupitia ushirikiano bunifu kama huu. Lengo letu ni kusaidia kuunda thamani halisi ya kiuchumi nchini Tanzania kwa kuwezesha ushirikishwaji mpana wa watu kifedha kupitia uwezeshaji biashara ndogo kwa kukidhi mahitaji ya kifedha ambayo hayajatimizwa.

"Makubaliano haya ni sehemu ya ahadi yetu ya dola trilioni moja kwa ajili ya kujenga uendelevu wa kifedha ifikapo mwaka 2030, ikilenga katika kupanua upatikanaji wa ajira, upatikanaji fedha/mitaji, miundombinu ya msingi na huduma kwa jamii zenye kipato cha chini katika masoko yanayoibukia," aliongeza Ofisa Mkuu wa Nchi wa Citi Tanzania na Mkuu wa Benki, Geofrey Mchangila.

Mkopo huo ni mwendelezo wa kazi ya awali ya DFC na Benki ya CRDB pamoja na USAID/Tanzania kusaidia biashara ndogo za Tanzania, ikiwamo dhamana ya Dola milioni 20 kusaidia utoaji mikopo kwa biashara ndogo zinazolenga kutoa huduma za elimu.

Pia kufanya kazi katika sekta zisizo rasmi na dhamana ya Dola milioni nne kupanua upatikanaji fedha kwa wanawake na vijana katika sekta ya afya.

Afrika ni eneo la kipaumbele katika uwekezaji wa DFC na ni eneo ambako uwekezaji mkubwa zaidi wa DFC unaelekezwa. Shirika hili kwa sasa limewekeza zaidi ya Dola bilioni 11 katika nchi mbalimbali barani Afrika.