Asilimia 28 ya wanawake Tanzania wametendwa ukatili wa kingono utotoni

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:05 AM Sep 28 2024
Mkurugenzi Mkazi wa Plan International, Jane Sembuche
Picha:Mtandao
Mkurugenzi Mkazi wa Plan International, Jane Sembuche

ASILIMIA 28 ya wanawake nchini wamefanyiwa ukatili wa kingono wakati wa utoto, wakati wasichana watatu kati ya 10 huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) ya Mwaka 2023, ikibainisha ukatili huo wa kingono hufanywa na watu wa karibu.

Katika kukabiliana na masuala hayo, Shirika la Plan International- Tanzania limezindua kampeni ijulikanayo kama ‘Sikia Sauti Zetu’ yenye lengo la kupaza sauti za wasichana.

Akizungumzia uzinduzi wa kampeni hiyo jana, Mkurugenzi Mkazi wa Plan International, Jane Sembuche, alisema itadumu kwa miaka mitatu na itajikita katika masuala ya uongozi na ushirikishwaji jamii ya kitanzania, ikiwamo kukabiliana na masuala ya ndoa za utotoni.

Alisema kampeni hiyo itasaidia kuwapa ujasiri wasichana kupaza sauti zao pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili na viongozi kuwa tayari kuzisikia na kuchukua hatua ili kushughulia masuala hayo.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu cha kampeni hiyo, wasichana 3,000 wanatarijiwa kufikiwa moja kwa moja ili kupewa elimu ya namna ambavyo wanaweza kushika nafasi za uongozi na wenye mamlaka pia kusikiliza sauti za kundi hilo.

"Hii si tu fursa ya kipekee kwa wasichana kujifunza, bali pia ni njia ya kujenga imani yao katika uwezo, tunahamasisha kushika nyadhifa mbalimbali kama vile wakurugenzi wakuu, mameya, mawaziri, Rais na nafasi nyingine za heshima, ili kupata ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao na kuwa na mtazamo kwamba wanaweza kufikia kile wanachokitamani," alisema Sembuche.

Alisema kuwa Oktoba 11 mwaka huu, Plan International itaungana na wadau kote ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Msichana (IDG) na jukumu lao litakuwa kuhamasisha na kutoa elimu ya upatikanaji haki na uwezeshwaji.

Alisema siku hiyo ni maalum kwao katika kutambua haki za wasichana na vikwazo wanavyokabiliana navyo na kuweka jitihada za makusudi kuwawezesha kupata haki na kutimiza malengo yao.

Baadhi ya mabalozi katika kampeni hiyo akiwamo, Mariam Surve, Ofisa Tabibu na Mchechemuzi wa Afya ya Akili, alisema ukata wa fedha ndani ya familia umechangia wasichana kukosa haki zao za msingi, ikiwamo elimu.

Tabibu alisema kuwa suala la afya ya akili ni muhimu kupewa uzito ili kuwawezesha mabinti kutimiza malengo yao.

Alisema kuwa wakiwa sawa kiakili, watakuwa huru kufanya mambo wanayoyakusudia.

Zafarani Ramadhan, mhitimu wa Shahada ya Kemia, Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM), alisema ni wakati wa kuhamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mwanafunzi mwingine chuoni huko, Felister Alex, anayesomea Shahada ya Mitindo, alisema wasichana wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto ikiwamo kunyanyapaliwa na kutengwa, jambo linalosababisha kushindwa kutumiza malengo yao kama kupata elimu.

Alisema kuwa kabla ya kusomea fani hiyo, alikuwa na ndoto ya kuwa daktari, lakini kwa sababu ni mtu mwenye ualbino, alikatishwa tamaa kwamba hawezi kufikia ndoto hiyo.

*Imeandaliwa na Grace Mwakalinga na Gwamaka Alipipi