JUZI kati hapa nikawa nimepata mwaliko wa harusi Dodoma, sikuwa na kisingizio cha kutokwenda, kwa sababu mwalikaji mwenyewe alishanikatia tiketi ya treni ya mwendokasi-SGR.
Shauku ya kutaka kupanda treni hiyo kwa mara ya kwanza, ikaongeza kasi ya kukubali kwangu mwaliko bila kusita na moyoni nikajipangia kuwa na akiba yangu kwa lolote, huwezijua nini kinaweza kutokea baadaye.
Tiketi yangu nikatumiwa kwenye simu, ikinionesha siku ya kuondoka na muda, ambao ni saa 12 asubuhi, nikitakiwa kufika stesheni ya Dar es Salaam saa 10 alfajiri. Nani akatae? Nikawahi kulala ili niwahi kudamka.
Nililala mang’amung’amu, unajua tena siku ya kwanza kupanda dude ambalo unalisikia tu sifa zake kwa watu waliolipanda na wengine wakiongeza chumvi, hivyo nikataka nami hiyo chumvi nikaionje kama inatosha au imezidi.
Siku ya siku alfajiri, huyoo na bajaji mpaka stesheni na kuwahi kuingia huku nikilakiwa na wafanyakazi nadhifu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), wakinielekeza kukaguliwa begi na vyote nilivyokuwa navyo, ikiwa ni pamoja na kuvaa mkanda na kisha kupanda juu ghorofa ya pili.
Eti ni kama kwenye ndege, ambayo sijawahi kupanda pia! Huko nako wengine wakinitaka nionyeshe tiketi, nikawaambia labda nikaichape kwa sababu iko kwenye simu! Ushamba bhana! Wakatabasamu tu na kuniambia ni hiyo hiyo ya kwenye simu. Kwa mshangao nikawapa, wakaitazamisha mahali kwenye kijiguzo hivi, nikaruhusiwa kuingia.
Nikidhani pengine ni wa kwanza kwanza kufika, aah wapi! Kumbe wenye shauku tuko wengi, kuna waliodamka kabla yangu wako kibao na viti ni vya kutafuta, kukaa kusubiri muda wa kuondoka. Nikapata kiti nikakaa huku shauku ikizidi kunilemea. Mgeni siku ya kwanza si mchezo.
Tukiwa hapo, mara tunatangaziwa kwenda kupanda, nababaika kidogo kujua behewa langu, lakini naulizia na natazamiwa kwenye simu yangu na kuambiwa ni namba fulani na kiti fulani. Hapo moyo unatulia, najifanya mwenyeji nakwea pipa la ardhini, najituliza kama si mshamba mimi.
Saa 12 asubuhi juu ya alama, nasikia honi na polepole ‘gogo’ linaanza kuondoka na kuchanganya kinoma. Ghafla anakuja binti akisukuma kijitoroli mithili ya kijikontena fulani hivi chenye maji ya chupa, soda na majagi ya chai na kahawa.
Anaanza kuniuliza mimi niliyekaa dirishani, namwomba anipe chai na korosho (zingatia naomba). Ananipa karatasi laini yenye vipakiti viwili kama sigara hivi, kumbe ni sukari, ananipa bilauri ya plastiki yenye majimoto na kijifuko chenye uzi, kumbe ni majani ya chai kisha kijipatiki cha korosho.
Najikorogea pale na kuchana kijipakiti cha korosho. Ghafla ananiomba fedha! Hapo sasa, tuliozoea mabasi ya peremende na maji bure, naona kama naumbuka hivi, sikudhani nalipia. Nashituka kimoyomoyo najikaza kuulizia bei, ananiambia “elfu nne tu baba”.
Naangalia ile bidhaa ya ‘elfu nne tu baba’, nguvu inaniishia, lakini nashika mfukoni kivivu na kutoa noti ya Sh 5,000 nampa, ananirudishia buku nalisondeka mfukoni huku sasa chai iliyowekwa sukari kama inageuka kuwa na shubiri.
Najipa nguvu, “potelea pwete,” najisemea huku nikiangalia jinsi gogo lile linavyochanja mbuga sijapata kuona, najisahaulisha buku nne zangu mara tunatangaziwa kufika Morogoro! Natazama saa, ni saa moja kama na dakika arobaini hivi, nashangaa.
Mahali ambako tulikuwa tukitumia saa nne mpaka tano, leo tunatumia saa moja na nusu na ushei kufika Morogoro?
Ukakasi wa chai unanitoka kabisa, najihisi kupata jambo la kusimulia siku nikirejea nyumbani.Dakika tano si nyingi, nasikia honi tena, hilo dude linatambaa kuitafuta Dodoma. Najifanya nimeshiba chai ile ya mang’amung’amu na kujipa matumaini ya kuvamia supu nifikapo Dodoma, kwa sababu harusi yenyewe ni jioni.
Kutokana na kudamka asubuhi, nikajikuta napitiwa na usingizi wa pono. Naota mauzauza mengi tu, yakiwamo ya ghorofa la Kariakoo kuporomokea ndugu zetu, kuwaua na wengine kuwajeruhi.
Ghafla nashitushwa na abiria jirani yangu ambaye tangu tuanze safari hatukuwa tumebadilishana hata chafya, ananiambia: “Ndugu yangu tumefika, amka.” Kweli nazinduka, naangalia saa ni saa nne kasorobo hivi. Nashangaa tena!
Mahali ambako awali tulitumia saa 10 kufika kwa basi, leo tunatumia saa nne tu, kweli? Hakika hii SGR iacheni iitwe SGR! Mbona ni mkombozi wa ajabu kwetu abiria tunaofanya safari za Dar-Moro na Dar-Dodoma na kurudi?
Kilichonishangaza zaidi, ni kumwona jamaa yangu fulani anayefanya kazi Mamlaka ya Usafiri wa Anga naye akiwa nasi na namsikia akisifia na kujiapiza kuwa ndege zitamsikia tu kwa SGR hii.
Tukashuka nikapanda bajaji hadi Area C kwa jamaa yangu, akanipokea na hakika jioni harusi ilikuwa nzuri.Baada ya siku mbili, nikarudi Dar es Salaam, safari hii kwa basi! Ya humo we acha tu, nitakusimulia tukionana. Wenye mabasi hamtaniona tena kwenye mabasi yenu hakika. Si kwa mateso niliyopata! Mpao waitu!
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED