Achomwa mshale ubavuni, kisa mgogoro ardhi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:50 PM Jan 22 2025
Mussa Ngassa, mkazi wa kijiji cha Nhobola, wilayani Kishapu, akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kuvamia na watu wanane na kuchomwa na mshale ubavuni.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mussa Ngassa, mkazi wa kijiji cha Nhobola, wilayani Kishapu, akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kuvamia na watu wanane na kuchomwa na mshale ubavuni.

Mussa Ngassa (39), mkazi wa kijiji cha Nhobola, wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, amenusurika kifo baada kudaiwa kuchomwa na mshale ubavuni, wakigombea ardhi.

Ngassa akizungumza na waandishi wa habari leo, katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, kupatiwa matibabu, amesema  Jumatatu, majira ya jioni, akitoka shambani, alivamiwa na watu wanane, miongoni mwa wenye mgogoro naye.

Amedai kwamba ana mgogoro wa ardhi na kwa muda wa miaka mitano na kwamba kesi ilipopelekwa mahakamani alishinda na kisha eneo hilo kukabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu.

“Hii ni mara ya nne nashambuliwa na watu hawa, siku moja walinipiga na panga kichwani, nikapelekwa hospitali nikapona, sasa hivi wamenipiga tena na mshale, naomba vyombo vya dola viwachukulie hatua watu hawa ipo siku wataniua kabisa,” amesema Ngassa.

Dada wa mwanamume huyo, Magreth Ngassa, amesema baada ya kupata taarifa ya kaka yake kupatwa na tukio hilo, alifika eneo hilo la mgogoro wa ardhi, kumchukua na kumkimbiza hospitali, huku watu hao wakikimbia kusikojulikana.

Daktari Kitengo cha Upasuaji Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Matinde Dotto, amesema walimpokea Ngassa akiwa katika hali mbaya, damu zikivuja huku kipande cha mshale kikiwa kimeingia hadi kwenye Ini, walifanikiwa kukitoa na hali yake inaendelea vizuri.

Mshale
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kwamba tayari wanamshikilia mtu mmoja kwa hatua za upelelezi, huku wakiendelea kuwatafuta watu wengine saba, ambao wanatuhumiwa kutekeleza tukio hilo.

Amesema kwa taarifa za awali, zimebaini chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi na kutoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.