Wakulima, wafanyabiashara wahimizwa kukata bima kukabiliana na majanga

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 05:41 PM Jan 22 2025
Wakulima, wafanyabiashara wahimizwa kukata bima  kukabiliana na Majanga.
Picha:Mtandao
Wakulima, wafanyabiashara wahimizwa kukata bima kukabiliana na Majanga.

WAKULIMA na wafanyabiashara wadogo nchini wameshauriwa kutumia bima ili wanapopatwa na majanga kwenye biashara zao au kwenye kilimo, bima hiyo itumike kufidia hasara za majanga kwenye shughuli zao hizo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya bima ya Newtan, Nelson Rwihula, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana.

Alisema yapo majanga mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwakumba wakulima ikiwamo yale ya mafuriko, mazao kuliwa na wadudu, au kuathiriwa na magonjwa, ukame na uharibifu mwingine na kwamba endapo mkulima akipatwa na hayo na akiwa ameyakatia bima, ni  rahisi kufidiwa na akanyanyuka tena kuendelea badala ya kukata tamaa.

“Si tu wakulima, hata wafanyabiashara wadogo, wanatakiwa wawe na bima ambayo inapotokea wakapatwa na majanga, inakuwa rahisi kufidiwa, ni vile tu kunakuwa hakuna elimu ya kutosha kwenye makundi hayo, lakini kulingana na shughuli zao hizo hizo hata kama ni ndogo wanasaidika, tena kulingana na kiwango chao hicho hicho,”alisema Rwihula.

Meneja wa Benki Bima, Frank Kajo, alisema tayari wamekuwa wakipata ushuhuda kwa baadhi ya wakulima ambao tayari wamepatiwa bima, namna ambavyo imewasaidia katika vipindi vigumu walipopata majanga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya Newtan, Nelson Rwihula na wadau wenzake wakiwa ameshika funguo kama ishara ya uzinduzi wa jina mpya la kampuni hiyo.
“Kwa hiyo wapo ambao walikumbwa na majanga ya mvua ya mawe mazao yakaharibika, wengine ilikuwa ni kutokana na magonjwa ya mazao, na majanga mengine, wote hao wamefidiwa na wameendelea tena na shughuli zao hizo,” alisema Kajo.

“Kwa mfano unakuta mkulima alikuwa anatakiwa kupata gunia 30 kwenye shamba lake, lakini kutokana na majanga, ameshindwa kupata, kwa hiyo kinachofanyika ni tathmini halafu anafidiwa ile hasara ili kumnyanyua tena asikate tamaa na akaacha kabisa kujishughulisha na kilimo.”

Alisema wakulima ambao wamekuwa wakiwasaidia kuwapatia bima hiyo, wengi wao ni kupitia vikundi vya Ushirika vya Kilimo na Masoko (AMCOS), na kwamba lengo la ni kuhakikisha wanatanua wigo kwa kutoa bima hiyo kwa wakulima wengi zaidi.

Mbali na mazao, Kajo alisema bima hiyo pia inalipa vifaa vyao pamoja na nyumba ambazo zinaharibika au kuteketea kutokana na majanga ya aina yoyote.