Wananchi warudisha matumaini kukamilika ujenzi daraja Same

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:48 PM Jan 17 2025
Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega akizingumza na wananchi baada ya kutembelea na kukagua miundombinu ya daraja lililobomoka Same.
Picha: Mtandao
Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega akizingumza na wananchi baada ya kutembelea na kukagua miundombinu ya daraja lililobomoka Same.

WANANCHI wanaotumia barabara ya Same Mkomazi wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kukamilika kwa ujenzi wa haraka wa daraja lililovunjika katika kijiji cha Mpirani, Same mapema mwezi huu kutokana na mvua.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameeleza kwamba kukatika kwa daraja hilo kulikata mawasiliano ya barabara kati ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro hadi Mkomazi hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwao.

“Tunamshukuru sana Rais kwa kumtuma Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega kuja hapa kuangalia hali na kutoa maelekezo. Tunashukuru kwamba daraja linapitika na tunaweza kuendelea na kazi zetu kama kawaida,” amesema Hassan Mkayanda ambaye ni mkazi wa Same.

1

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alitembelea eneo hilo wiki iliyopita na kuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kujenga daraja hilo usiku na mchana ili liweze kupitika tena na kuruhusu shughuli za kijamii na kiuchumi zirejea katika hali ya kawaida.

Barabara hiyo muhimu katika upande wa Kaskazini mwa Tanzania ni miongoni mwa zilizoathiriwa na mvua ambazo Waziri Ulega alizifanyia ukaguzi katika maeneo tofauti nchini kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita.