Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa (76), leo Januari 17, 2025 amefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kusikikiza kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili.
Dk.Slaa alifikishwa mahakamani hapo Januari 10, 2025 akikabiliwa na kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025, ambapo alitarajiwa kufikishwa mahakamani hapo Januari 13, 2025 kwa ajili ya kujua hatma ya dhamana yake baada ya Upande wa Jamhuri kuwasilisha kiapo cha kuzuia dhamana.
Wakili wa Serikali, Issa tawabu alisema kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya mjadala wa dhamana lakini mtuhumiwa hakufika mahakamani licha kwamba alitakiwa kufika na akisisitiza kuwa wameuliza lakini wameambiwa hajafika.
Kutokana na mvutano wa kutofikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa na hatma ya dhamana yake, huku hoja nyingine zikiibuka kutoka pande zote mbili za Mawakili wa Serikali na Utetezi, Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi leo Januari 17, 2025.
Dk.Slaa alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X, akidaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015 akidaiwa kutenda kosa hilo Januari 9, 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED