Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva ameongoza wananchi wa Kata ya Nangaru- Lindi Manispaa kwenye zoezi la uchimbaji wa misingi ya majengo ya shule mpya ya Sekondari ya Amali ambayo inapewa jina la Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Secondary School.
DC Victoria amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa miradi ya maendeleo kwenye Sekta ya Elimu; Lindi Manispaa na kwa kutoa shilingi 560,552,827/= kupitia mradi wa SEQUIP III ili kufanikisha Ujenzi wa shule hii mpya.
"Hamasa ya kujitolea nguvu za wananchi ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Sania kwa kuleta huduma hii ya elimu kwa ukaribu zaidi na wananchi ili kuepusha safari ndefu ya kufuata shule kata jirani. Viongozi wa Serikali za Vijiji- Kata, Sambamba na viongozi wa Chama wamejitokeza kwa wingi na wanachi wa Nangaru ili kuwezesha zoezi hili la uchimbaji wa msingi ili kuendelea na ratiba za Ujenzi."
Katika hatua nyingine, amesisitiza ubora wa mradi, ufanisi na weledi wa usimamizi ili kupata mradi wenye kuakisi thamani ya fedha na wenye kuhudumia vizazi na vizazi.
DC huyo amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kujitolea nguvu zao na kuleta hamasa kubwa katika shughuli hii ya awali ya uchimbaji msingi amezidi kushukuru na kuomba ushirikiano wao kwa hatua zote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED