Asiyefahamika atoweka na mtoto wa miaka miwili Morogoro

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 05:00 PM Jan 17 2025
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama.

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamsaka mtu asiyefahamika kwa tuhuma za kumteka mtoto Shamimu Ndihagule mwenye umri wa miaka miwili. Mtoto huyo aliibwa kutoka kwa wazazi wake wanaoishi katika Kitongoji cha Kisiwani, Kijiji cha Tunda, Kata ya Kidodi, Tarafa ya Mikumi, Wilaya ya Kilosa, mkoani humo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amethibitisha tukio hilo, akisema lilitokea majira ya asubuhi ya Januari 15, 2025. Mtoto huyo alichukuliwa na mtu huyo wakati akicheza na mtoto mwenzake Josephat Jangama mwenye umri wa miaka mitatu, mkazi wa kitongoji hicho.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkama, taarifa zinaeleza kuwa wakati watoto hao wakiwa wanacheza, mtu huyo asiyejulikana alitokea ghafla na kumchukua Shamimu, kisha kutokomea naye katika mashamba ya miwa.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo, tumeanzisha msako mkali ambao unaendelea hadi sasa. Tunawaomba wananchi wote wenye taarifa zitakazosaidia kumpata mtoto huyo wazipeleke katika kituo chochote cha Polisi au ofisi nyingine yoyote ya serikali,” amesema Kamanda Mkama.

Mlemavu wa Ngozi Afariki Kwa Kuanguka Juu ya Mnazi

Katika tukio jingine, Rashid Mussa (24), mwenye ulemavu wa ngozi na mkazi wa Kitongoji cha Kimbawala, Kijiji cha Kiziwa, Kata ya Kiroka, Wilaya ya Morogoro, amefariki dunia baada ya kuanguka kutoka juu ya mnazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro amethibitisha kifo hicho, akieleza kuwa taarifa za awali zilitolewa Januari 13, 2025, zikihusu kutoweka kwa kijana huyo kutoka makazi ya baba yake, Juma Mussa Juma (45), mkulima na mkazi wa kitongoji hicho.

Kamanda Mkama amesema kuwa baada ya kupokea taarifa hizo, Polisi walifanya ufuatiliaji wa kina. Mnamo Januari 15, 2025, majira ya alasiri, mwili wa Rashid Mussa ulipatikana chini ya mti wa mnazi mrefu, huku pembeni yake kukiwa na nazi 14 zilizokuwa zimeanguliwa kutoka kwenye mnazi.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu alianguka kutoka juu ya mnazi na kufariki papo hapo wakati akiangua nazi kwenye mashamba ya nazi,” ameongeza Kamanda Mkama.